Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imefanikiwa kujenga ghala bora la kisasa kwa wakulima wa vitunguu na ukarabati wa barabara vilivyogharimu kiasi cha bilioni 3 katika kijiji cha Mang’ora.
Akitoa taarifa hiyo kwa timu ya ukaguzi kutoka taasisi ya Marketing Infrastricture,Value Addition and Rural Finance Support ( MIVARF) na Benki ya maendeleo Afrika, Mkurugenzi wa halmashauri bwana Waziri Mourice amesema halamshauri yake imefanikiwa kutoa 5% katika ujenzi wa ghala la vitunguu na ukarabati wa barabara.
“Kweli tumejitaidi sana kama halmashauri kutoa 5% ya makusanyo yetu ya ndani na kufanikisha ujenzi wa ghala na ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomita 27”.
Ukarabati wa barabara katika bonde la Eyasi umegharimu kiasi cha bilioni 1.5 na ujenzi wa ghala umegharimu kiasi cha bilioni 1.5 ambapo na halmashauri ilichangia milioni 153.
Amesema ghala hilo limekuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima kwa kuwaunganisha kwa pamoja kupitia chama chao,pia ghala hilo litawawezesha wakulima kupanga bei moja ya manunuzi na kuwawezesha kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.
Bwana Waziri ameishukuru MIVARF kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha shughuli hizo za maendeleo katika halmashauri hiyo na kuomba zaidi ushirikiano katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mahindi,kufufua kiwanda cha kusindika maziwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Akifafanua zaidia bwana Salum Ramadhani mtaalamu wa mambo ya kilimo kutoka Benki ya maendeleo Afrika,amesema lengo la timu hiyo kutoka MIVARF makao makuu ni ukaguzi wa miradi inayofahiriwa na taasisi hiyo ambao unafanywa kila baada ya miezi 6.
Amesema mradi wa ghala la vitunguu ulilenga zaidi kuweka utaratibu wa kuwa na soko la pamoja kwa wakulima wenyewe wa vitunguu na hii itasaidia kupunguza uuzaji wa kiholela kwenda nchi jirani.
Ameipongeza halmashauri kwa kufanikiwa kutoa asilimia 5 ya mapato yake katika ujezi wa ghala hilo na ukarabati wa barabara kwani ni halmashauri nyingi zimeshindwa kufanya hivyo.
Aidha, amewashauri wakulima kutafuta masoko ya vitunguu vyao kwa kutafuta taarifa za bei na masoko kutoka sehemu mbalimbali ili wawe na uweleza mpana zaidi.
Mwenyekiti wa halmashauri mheshimiwa Jublate Gerson Mnyenye amesema Changamoto kubwa wanayoipata kama halmashauri ni ujazaji wa maguni kwa lumbesa inayopelekea wakulima kupata hasara.
Hata hivyo amesema bado wakulima wa vitunguu wanachangamoto ya mafuriko kuingia kwenye mashamba yao inayopelekea hasara kwa kupata mavuno hafifu.
Bado halmashauri inaendelea kuandaa utaratibu wa kuwasaidia wakulima kuweza kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kwenye ghala.
Akisisitiza zaidi mratibu wa MIVARF upande wa miundombinu ya masoko Bwana Jacob Mwambene amesema, wakulima hao wanatakiwa kulitumia hilo ghala kama malengo yalivyokusudiwa kwa kuwa mradi huo ulilenga kumwinua mkulima mdogo na wakati katika kilimo cha vitunguu.
Nae katibu wa chama cha wakulima wa vitunguu (LECOFANET) Elia Bacheng, amesema bado kuna uhaba wa visanduki vya kuwekea vitunguu kwani vilivyopo havikidhi mahitaji ya sasa.
Aidha,wameiomba serikali iongeze mizani yakupimia magunia yanapokuwa yanaingia katika ghala hilo .
Pia Changamoto nyingine ni kutokuwa na bei maalumu kwa uuzaji wa vitunguu kwani wanaopanga bei kwa sasa ni madalali ambao baadhi yao ni wakulima wenzao inayopelekea wakulima kuuza vitunguu vyao kwa hasara.
Ujenzi wa ghala la vitunguu lilifunguliwa rasmi Novemba 2017 kwa lengo la kuwasaidia uuzaji wa vitunguu kwa wakulima wa vijiji vya Mang’ola na Baray kuwa na soko moja la pamoja na ujenzi wake umefadhiliwa na taasisi ya MIVARF kwa kushirikiana na halmshauri ya wilaya ya Karatu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa