Na Elinipa Lupembe
Wananchi na wakazi wa Kijiji cha Laja kata ya Ganako, wilaya ya Karatu, wamemshukuru Rais Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajengea shule mpya ya Sekondari Laja, shule iliyowapushia gharama za kuwapangia watoto wao vyumba maarufu kama 'mageto' wakati wakienda kusoma kata za mbali.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wananchi hao wamesema kuwa, Serikali kujenga shule katika eneo lao, shule ambayo licha ya watoto wao kupata elimu, wamekiri kuwapunguzia wazazi mzigo wa gharama za kuwapangia vyumba (mageto), miaka yote wakiwa shuleni
"Ilikuwa mtoto akipangiwa sekondari, tulilazimika kuwapangia vyumba karibu na shule huko Laansey, ilikuwa na gharama kubwa pamoja na usalama mdogo kwa watoto, zaidi wazazi wengi hawakuweza kumudu gharama hizo na watoto kulazimika kutembea umbali mrefu" Wamesema wananchi hao.
Wamesema kuwa, watoto wao wamepata fursa ya kusoma ndani ya eneo lao, wakati hapo awali walitembea zaidi ya Km 10 -16 kwenda na kurudi shuleni, jambo lililosababisha utoro kwa wanafunzi sambamba na baadhi kuacha shule kutokana na utoro na mimba za utotoni kwa wasichana.
Rehema Matley Amey, amesema kuwa, Serikali ya mama Samia imefanya miradi mingi katani hapo, imejenga shule ambayo imewaondolea kero na changamoto watoto ambao walitembea umbali mrefu huku kipindi cha mvua wakikosa masomo kutokana na makorongo kujaa maji lakini sasa changamoto hizo hazipo, shule imejengwa na daraja limejengwa hakuna tena watoto kukosa masomo.
"Tunaishukuru mama Samia kupitia TASAF, ilianza kwa kujenga daraja na shule ikafuata, watoto wetu waliishi kwenye nyumba za kupanga mitaani 'mageto' wakati wanasoma Kansay huku watoto wakiishi bila usimamizi jambo ambao wasichana walifanyiwa vitendo vya ukati na wengine kuacha masomo kwa kupata mimba za utotoni" Amesema Mama Rehema
Hata hivyo, wanafunzi wa shule ya Sekondari Laja, hawakuwa nyuma, wamemshukuru Mama Samia kwa kuwajengea shule, huku wakijipongeza na kujivunia kwa kuanzisha shule mpya na kumuomba Mheshimiwa Rais kuwajengea Hosteli kwa kuwa bado wapo wanafunzi wanaotoka mbali na shule ilipo.
Emmanuel Fanueli, amesema kuwa anajivunia kwa kuwa wanafunzi wa kwanza kwa kuanzisha shule hiyo ya Laja, nakumuahidi Mama Samia kusoma kwa bidii huku akimuomba Mama Samia kuwajengea Hosteli ili wanafunzi waweze kulala shuleni.
"Tunamshukuru rais Samia ametujali watoto wa kike Laja, wengi waliacha shule kutokana na mimba za utotoni lakini uwepo wa shule hii hapa jirani, tunamuadi Rais kusoma kwa bidii na kuwa Mwalimu" Amesema Elizabeth Mathay Niima.
Mkuu wa shule ya Sekondari Laja, Mwl. Daniel Awey Panga, amesema kuwa shule hiyo imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 333.3 fedha kutoka Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF - OPEC IV), shule ambayo tayari wanafunzi 25 wa kidato cha kwanza, wameanza masomo mapema Januari 2024.
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa