Na Elinipa Lupembe
Kata ya Sale, iko umbali wa takribani Kilomita 49 kutoka makao makuu ya wilaya ya Ngorongoro yaliyoko eneo la Waso kata ambayo ina wakazi 6,579, wanaojishughulisha na kilimo na ufugaji.
Kwa kipindi kirefu, hawakuwahi kuwa na kituo cha afya, zaidi walikuwa na zahanati ndogo ya kijiji, ambayo ilitoa huduma ambazo, kutokana na ongezeko la idadi ya watu, ilifikia kuelemewa na kushindwa kutoa hudmua stahiki kwa wote.
Wananchi wa Sale hususani wanawake, walilazimika kwenda eneo la Waso, kupata huduma za kujifungua jambo ambalo liliwagharimu muda na fedha na kusababisha vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua, kutokana na ucheleweshwaji wa upatikanaji wa huduma.
Jenifa Ismael Legina, licha ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kujenga kituo cha afya Sale, amethibitisha, kituo hicho kitaondoa vifo visivyo vya lazima, hasa kwa wanawake wakati wa kujifungua kwa kuwa, kinatoa huduma bora huku kikiwa na madaktari wazuri wenye moyo wa kuwahudumia.
"Kuna wajawazito walipoteza maisha kwa kukosa huduma ya kuongezewa damu, ilikuwa mpaka uenda Waso, kama huna pesa, ilikuwa ni tatizo kwa familia nyingi, wakati mwingine tulilazimika kuchangishana ili mtu akapate huduma, kwa sasa hakuna tena hayo maisha" Ameweka wazi Jenifa.
Naye Bi. Hosiana, mama wa watoto watatu ambaye ni mgonjwa wa kwanza kujifunga katika wodi ya wazazi, amesema , watoto wake wawili alilazimika kufunga safari mpaka Waso, umbali wa zaidi ya Km 49 kutoka eneo hilo, ili kwenda kujifungua jambo ambalo liliwapa gharama kubwa za fedha na muda, lakini wapo kinamama waliopoteza maisha kwa kuchelewa kupata huduma za kujifungua.
"Ninamshukuru mama Samia, nimekuwa wa kwanza kulazwa kwenye wodi moya ya wazazi, ninamuombe aendelee kutuongoza watanzania, matunda yake tunayaona hadi huku vijijini"Amesema Hosiana.
Serikali ilitoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa zahanati ya Sale ili kuwa na hadhi ya kituo cha afya, na tayari kituo kimeanza kutoa huduma kwa jamii.
#TupoKazini
#tutakufikiapopoteulipo
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa