Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Idd Hassan Kimanta amewasimamisha kazi Mtendaji Kijiji na kata ya Mwandeti,na Afisa Tarafa ya Mukrati kuwa chini ya ungalizi ili kupisha uchuguzi zaidi na hatua kali zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.
Maamuzi hayo yamefanyika katika kikao kazi kati ya Mkuu wa Mkoa na maafisa tarafa 3 wa halmashauri ya Meru, watendaji wa kata 26 na vijiji 90 pamoja na wakuu wa idara na vitengo katika halmashauri hiyo.
Aidha Mheshimiwa Kimanta amesema kuna uzembe mkubwa umefanyika katika utendaji wa majukumu yao, hasa kushindwa kudhibiti kilimo cha bangi katika maeneo yao.
“Haingii akilini tokea bangi inalimwa kwa miezi 3 na mwezi wa 4 inavunwa wewe mtendaji wa kata na kijiji upo hapo na hauchukui hatua yoyote”.
Amesema haieleweki kwanini nyie kama viongozi mmeshindwa kudhibiti kilimo cha bangi kwa muda wote huo na mpo hapohapo.
Amewataka watumishi kuacha kufanyakazi kwa mazoea kwani dhama hizi niza kuwajibika kila mtu kwenye nafasi yake.
Kimanta amesisitiza zaidi kwa viongozi wa kata na vijiji kuwafichua wote wanaolima bangi katika maeneo yao badala ya kuwaficha,amesema kwa kufanya hivyo wanachangia kuiaribu jamii.
Amewataka viongozi hao wa kata na vijiji kutatua kero za wananchi katika maeneo yao hivyo watakuwa wamewatumika vyema wananchi wao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Arumeru Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Jerry Muro, amesema tatizo kubwa kwa watumishi wa wilaya hiyo ni kufanya kazi kwa mazoea ndio maana wanashindwa kuchukua hatua mbalimbali za kiutendaji katika maeneo yao.
Aidha, Muro amewataka watumishi wote kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali wawe wabunifu zaidi katika kutekeleza majukumu yao badala ya kuwasubiria viongozi wa ngazi ya juu tu.
Mheshimiwa Kimanta amefanya ziara fupi katika wilaya ya Arumeru, baada ya maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari John Pombe Magufuli dhidi ya tuhuma za ulimaji bangi katika wilaya hiyo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa