Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daktari Wedson Sichawe amewataka wazazi na walezi wote wenye Watoto chini ya miaka 5 kuwapeleke Watoto wao kupata chanjo mbalimbali.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa Habari wa Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga kwa lengo la kuwapa uwelewa mpana wa namna ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo kwa Watoto na wasichana wa miaka 14, Jijini Arusha.
Amesema kiwango cha chanjo kwa Mkoa wa Arusha kipo vizuri japo kwa kipindi hiki ambacho dunia imekubwa na ugonjwa wa Corona utoaji wa chanjo umepungua sana.
Daktari Sichawe amesema mtoto akikosa chanjo hizo anakuwa katika mazingira hatarishi zaidi kwa kuambukizwa magonjwa mbalimbali.
Aidha, wasichana wenye umri wa miaka 14 wao pia wanatakiwa kuendelea kupatiwa chanjo ya Saratani ya shingo ya Kizazi.
Akitoa ufafanuzi juu ya hali ya chanjo Afisa mpango wa Taifa wa Chanjo bi. Lotalis Gadau amesema, kwa sasa kiwango cha chanjo kimeshuka kwasababu wazazi wegi wameogopa kuwapeleka Watoto wao kwenye chanjo kutokana na ugonjwa wa Corona.
Amewataka wazazi na walezi kutotumia ugonjwa wa Corona kama sababu ya kutowapeleka Watoto kupata chanjo kwani mtoto aliye chanjwa ana kuwa na kinga kubwa dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Amesisitiza zaidi kuwa madhara yatokanayo na mtoto kukosa chanjo ni makubwa sana ikiwemo kupata magonjwa kama vile;Nimonia, degedege, mtindio wa ubongo, utapiamlo, matundu kwenye Moyo, ugonjwa wa Moyo na ulemavu wa viungo.
Bi. Lotalis amesema, ili mtoto aweze kuepuka magonjwa hayo inabidi apatiwe chanjo zote kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na pia kwa mabinti wa miaka 14 nao wapate chanjo ya Saratani ya shingo ya kizazi zote mbili.
Pia, amesema chanjo zote zinapatikana bure na hazina madhara yoyote kwa mtoto au msichana kwani zimethibitishwa na mamlaka ya dawa na vifaa tiba Tanzania (TMDA) na shirika la afya duniani.
Amevishauri vituo vyote vya afya vinavyotoa chanjo hizo kuhakikisha wanapanga ratiba rafiki ya chanjo ili kupunguza msongamano wa watu na kwa Watoto wasio na chanjo wanashauriwa kuhudhuria kliniki kila baada ya miezi 3, hii yote itasaidia kupunguza msongamano katika vituo hivyo hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakishirikiana na mikao hiyo minne ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa