Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amewahakikishia wadau wa sekta ya habari kuwa sekta ya habari ipo kwenye mikono salama.
Hayo yamesemwa leo Jumatano, tarehe 19 Juni, 2024 wakati akifunga Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari lililofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 18 hadi 19 Juni, 2024, kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mhe. Nnauye ameeleza kuwa kongamano hilo limewaunganisha wadau wote wa sekta ya habari na limechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ukuaji wa sekta ya hiyo.
“Wanahabari niwahakikishie kuwa sekta ya habari ipo mikono salama. Tuweke utamaduni wa kujadiliana vitu vitakavyoleta maendeleo katika nchi yetu. Kwa siku mbili tulizokuwa hapa tumejenga misingi bora zaidi, tumepata fursa ya kujadiliana mambo mbalimbali”
Alifafanua kuwa sekta ya habari ni muhimu katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa, hivyo wanahabari wakiamua, wanauwezo wa kurahisisha na kuchochea maendeleo ya Taifa kwa kasi zaidi.
Pia Mhe. Nnauye ameishukuru Kamati aliyoiundwa kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari ikiongozwa na Bw. Tido Mhando kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuahidi kuwa yote yaliyowasilishwa kwenye ripoti yao yatafanyiwa kazi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa