Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Musa, ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuimarisha usafi wa mazingira ili kuvutia watalii na kusimamia kwa ufanisi wakandarasi wa usafi na kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa staha bila kuleta malalamiko.
Akizungumza leo Juni 12, 2025 kwenye mkutano maalum wa baraza la madiwani wa mapitio ya hoja za ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2023/24, ambapo halmashauri hiyo imepata hati safi, Musa ameipongeza kwa kufuta hoja 30, kujadili hoja 20 na hoja 3 za zamani na kusisitiza hoja zilizobaki zifutwe ili kupunguza ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Pia amepongeza halmashauri kwa urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo hadi sasa zimerudishwa Shilingi milioni 915.5 kati ya Shilingi bilioni 1.38 na kuagiza kuimarishwa kwa usimamizi na urejeshaji wa mikopo hiyo.
Aidha, Mkaguzi wa Nje wa Mkoa wa Arusha, Valence Rutakyamirwa, ameshauri halmashauri kuweka mikakati ya kupitia hoja za nyuma, huku akisisitiza ukaguzi ujao uoneshe taarifa sahihi za matumizi ya fedha na utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu, Juma Hokororo, ameomba ushirikiano zaidi kutoka kwa watumishi katika ukusanyaji wa mapato na uboreshaji wa usafi wa mazingira.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa