Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa Jumla ya Shilingi Bilioni 14.4 kama fidia kwa Wakazi wa Vijiji vinne vilivyopo kwenye Kata ya Engaruka Wilayani Monduli Mkoani Arusha ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya sita katika uendelezaji wa miradi ya Kimkakati yenye tija kwa Taifa.
Kwaniaba ya Rais Samia leo Alhamisi Januari 23, 2025, Waziri wa Viwanda na biashara Mhe. Dkt. Seleman Jaffo wakati akizindua ugawaji wa fidia hizo kwa awamu ya kwanza yenye takribani Bilioni 6.2, amewataka wasimamizi wa zoezi hilo kuhakikisha kuwa ulipaji wa fidia hizo unamalizika kabla ya Februari 15, 2025, na kuaigiza shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kushughulikia malalamiko yote ya ya fidia kwa wananchi wa eneo hilo.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo aliyeambatana na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Wizara ya ardhi Mhe. Jofrey Pinda, amesema serikali imeweka mpango maalum wa kuhakikisha kuwa eneo la Engaruka linakuwa na barabara zinazopitika muda wote sambamba na upatikanaji wa umeme mkubwa wa Kilowati 33 ili kusaidia katika shughuli za uendeshaji wa viwanda viwili vikubwa vinavyotarajiwa kutekeleza mradi huo.
Akizungumza katika Uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda, amesema Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye bahati na kadri siku zinavyosonga, Mkoa huu utatoa fursa mbalimbali za maendeleo kwenye sekta za Kilimo, Madini na Michezo, zitakazosaidia wananchi kujikwamua na umaskini akihimiza kuendelea kupewa kipaumbele cha ajira kwa wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Arusha.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa Kimkakati, Mkurugenzi mwendeshaji wa NDC Dkt.Nicolaus Shombe amesema mradi huo wa magadi soda umechukua zaidi ya miaka 29 tangu mchakato wake ulipoanza baada ya NDC kufanya utafiti wake na kubaini uwepo wa magadisoda yenye kufikia mita za ujazo Bilioni 3.8 sawa na tani Milioni 787 ambapo kupitia utekelezaji wake, viwanda viwili vikubwa vitakavyogharimu Trilioni 1.6 vitajengwa katika eneo hilo lenye jumla ya ekari 60, 884.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa