Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Jumatano Februari 19, 2025 Ofisini kwake Jijini Arusha, amekutana na kuzungumza na Kamati ndogo ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania BAMMATA, ambao wanatarajia kufanya mashindano ya michezo ya Majeshi Jijini Arusha Mwezi Juni- Julai mwaka huu.
Katika mazungumzo yao, Mhe. Makonda ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mashindano hayo, akisema ni fursa adhimu kwa wakazi wa Arusha kuendelea kunufaika kiuchumi kupitia ugeni utakaokuwa unashiriki mashindano hayo yanayoandaliwa na kuratibiwa na BAMMATA suala ambalo pia litasaidia kuimarisha Ulinzi na usalama wa Mkoa wa Arusha kwenye kipindi chote cha Mashindano hayo makubwa ya Kijeshi.
Kwa Upande wake Viongozi wa Kamati hiyo ndogo wakiongozwa na DCF Kennedy Komba, Makamu Mwenyekiti wa BAMMATA na Kanali David Luoga, Katibu Mkuu wa BAMMATA, wamesema wameichagua Arusha kuwa Mwenyeji wa Mashindano hayo kwa mwaka huu kutokana na Ari na Hamasa iliyopo Mkoani humo inayotokana na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Christian Makonda.
Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) ni chombo cha kitaalamu cha michezo kilichosajiliwa kihalali kwa lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za michezo kwa Vyombo vya Ulinzi, Usalama na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).Baraza hili lilianzishwa rasmi mwaka 1977, Likijumuisha kanda nane ambazo ni Kanda ya Ngome, kanda ya JKT, Kanda ya Polisi, Kanda ya Magereza, Kanda ya Uhamiaji, Kanda ya Zimamoto, Kanda ya Visiwani na Kanda ya SMZ ikiwa na dhima ya Kudumisha michezo ya vyombo vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ili viwe vitalu vya maendeleo ya michezo nchini.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.