Benki ya NMB imetoa dawa za aina mbalimbali za binadamu zenye thamani ya takribani Shilingi Milioni 10 za Kitanzania, kusaidia wahitaji mbalimbali kwenye Kambi ya Matibabu ya kibingwa inayoendelea kwenye viwanja vya Michezo vya Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Bw. Praygod Godwin Meneja wa Tawi la Clock tower Jijini Arusha kwaniaba ya Meneja wa kanda ya Kaskazini wa Benki ya NMB amekabidhi dawa hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ambapo pia wametoa gari moja ya kubebea wagonjwa ili kusaidia wagonjwa watakaokuwa na uhitaji wa dharura ya kuwahishwa hospitalini.
"Kama mnavyofahamu NMB ni benki ambayo tunahusiana na jamii na tumehusika pia kwenye kutoa madawati na vifaa tiba kwenye hospitali mbalimbali na tunachofanya ni kurudisha kwenye jamii kwani tunaamini kuwa jamii inapokuwa na afya bora, wanapata nafasi ya kuzalisha na sisi ndipo tunapopata wateja.", amesema Bw. Praygod.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Makonda, ameishukuru benki hiyo kwa kujali na kujitoa kwaajili ya wananchi kwa kuthamini uhai wa binadamu, akihimiza wananchi wa Arusha kuendelea kutumia huduma za Benki hiyo ili kuchochea benki hiyo kuendelea kujitoa kwa jamii ya Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa