Wazazi na walenzi wametakiwa kuhakikisha wanasimamia Sera na Miongozo ya ulinzi wa watoto ili kujenga kizazi kinachojiamini na kujitambua katika ujenzi wa Taifa letu.
Ameyasema hayo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta alipokuwa akizindua kitabu cha Sera na Miongozo ya ulinzi wa watoto cha kanisa Katoriki la Arusha,katika kanisa la Mtakatifu Theresia, jijini Arusha.
Amesema jukumu kubwa la kumlinda mtoto linaanzia katika ngazi ya familia,hivyo wazazi ndio wenye jukumu kubwa sana la kuhakikisha watoto wao wanakuwa katika mazingira yenye usalama.
Kimanta amesema, kwa kufanya hivyo tutakuwa na taifa lenye watoto wanaojitambua,kujiamini na watakuwa na uwezo mkubwa wa kujielezea jambo lolote hususani hata wakifanyia ukatiri.
Juhudi zilizoonyeshwa na Kanisa hilo hazina budi kuungwa mkono na serikali kwani kwa kufanya hivyo ni kizazi kikubwa kitakombolewa.
Aidha, amewataka waumini wote wa Kanisa Katoriki kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha Sera hiyo ya ulinzi wa mtoto inatekelezeka kuanzia katika ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla.
Amesema moja ya changamoto ambayo inayowaathiri watoto kwa kiwango kikubwa ni mafarakano ya wazazi katika ndoa, hivyo kupelekea wahanga wakubwa kuwa ni watoto.
Nae, Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Katoriki la Arusha Isaac Amani amesema, watoto wanahaki ya kutunzwa, kuthaminiwa na kupendwa kwani wanaitaji kuelekezwa ni kwa namna gani wanaweza kukabiliana na changamoto zao.
Amesema amani yetu katika nchi ndio nguzo inayosaidia kuweza kuwalea watoto katika mazingira ya amani na utulivu.
Amesisitiza kuwa kuanzi sasa watumishi wote wa katisa Katoriki la Arusha wanaoshughulika na maswala ya watoto watatakiwa kisaini makubaliano ya namna ya kuitekeleza Sera hiyo katika maeneo yao ya kazi, ili kuhakikisha Sera hiyo inafanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Akielezea malengo ya Sera hiyo Mratibu wa maandalizi ya uundwaji wa Sera na miongozo hiyo Padre Dennis Ombeni Ngowi amesema, Sera na miongozo hiyo ni kwa ajili ya kumlinda mtoto.
Pia, kuweka mazingira bora ya malezi kwa mtoto, kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na manyanyaso kwa watoto katika hatua zao mbalimbali za makuzi.
Amesema Sera hiyo itasaidia kuweka mazingira mazuri ya upatanishi katika changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto.
Kanisa Katoriki jimbo kuu la Arusha, limezindua Sera na miongozo ya ulinzi wa mtoto baada ya kubaini kuwa watoto wengi wanapitia manyanyasa na ukatiri bila jamii kuwa na uwelewa mpana.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa