Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameunda Tume Maalum ya kufuatilia Malalamiko ya wananchi pamoja na zuio la kujengwa kwa machinjio ya Ngorbob, yaliyopo kwenye Kata ya Matevesi, halmashauri ya Arusha Wilayani Arumeru.
CPA Makalla ametoa maelekezo hayo leo Jumanne Septemba 09, 2025 wakati wa Kikao kazi na Viongozi wa serikali za Mitaa na Vijiji pamoja na watendaji wa Kata na Vijiji vya Wilaya ya Arumeru, akishangazwa na malalamiko hayo ambayo yamekuja baada ya mradi kukamilika.
"Hili jambo lazima tulimalize, nitaunda Tume ya kufuatilia mchakato ulivyoanza na mpaka ulivyokamilika na kwanini mradi huu uwe haufai sasa, ulianzaje, makubaliano yenu yalikuwaje. Ile tume isihusishe watu wa Arumeru, watoke watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na isimuhusishe Afisa Biashara wa Mkoa ili kuepusha muingiliano wa maslahi. Tume hii itafanya kazi ndani ya wiki mbili, tujue pia wananchi walihusishwa ama hawakuhusishwa, sheria za mazingira zilizitangatiwa? na kwanini muwekezaji awali aliruhusiwa kuanza ujenzi wa mradi." Amesema Mhe. Makalla.
Kulingana na maelezo ya CPA Makalla, Muwekezaji wa Machinjio hayo alipewa eneo hilo na Halmashauri ya Arusha Dc na kutumia zaidi ya Milioni 800 kwaajili ya ujenzi wa mradi huo baada ya wataalamu wa mazingira kueleza kuwa hakuna athari za mazingira katika utekelezaji wa mradi huo, akiagiza uchunguzi ufanyike kujua uhalali wa machinjio hayo na makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa hapo awali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa