Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella, amekemea tabia ya wahandisi kuletewa fedha za miradi kutoka Serikali Kuu na kutokukamilisha mradi kwa fedha hizo na baadaye kupanga kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani.
Amesema hayo mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya kata Mundarara wilaya ya Longido na kupewa tarifa ya fedha zilizotolewa na serikali milioni 470, haziweza kukamilisha mradi huo na kupanga kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani.
Mhe. Mongella licha ya kuuagiza uongozi wa wilaya ya Longido kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa maeneo madogo yaliyosalia ifikapo Desemba 15, mradi ukuwa umezingatia vigezo vya ubora vilivyoainishwa na Serikali, na kuwasisitiza kuhakikisha fedha zilizotolewa na Serikali Kuu, zinakamilisha mradi huo bila kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani.
Aidha amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Marco Ng'umbi kuwasimamia watendaji wote wa chini yake, kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa fedha zilizoletwa na Serikali na si vinginevyo kwa kuwa fedha zote zinakuja zikiwa na maelekezo yake.
"Fedha za Mapato ya ndani tayari zina mpango wa bajeti ya matumizi yake, mnapoingiza matumizi
mengine nje ya bajeti mnasababisha kuua kazi zilizopangwa na kusafanya shughuli na mipango ya halmashauri kupitia mapato ya ndani kukwama na kushindwa kufikia malengo" Amesema Mhe. Mongella
Aidha amewataka watendaji wote wa Serikali na viongozi wa wananchi, Baraza la Madiwani na Kamati ya fedha, kubadilika katika usimamizi wa miradi, serikali imewapa dhamani ya kusimamia shughuli za serikali ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii kisekta kama yalivyo malengo ya Serikali.
"Tuweni wazalendo kwa kuwahurumia na kuwasaidia watoto wetu, watoto wa kitanzania hawana hatia, kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi hii ya elimu, watoto wetu wanakwenda kunufaika nayo" Ameweka wazi Mhe. Mongella
Awali Serikali kupitia programu ya Kuboresha Miundombinu ya Shule za Sekondari Nchini (SEQUIP), imetoa shilingi milioni 470 za kujenga shule mpya ya sekondari ya kata ya Mundarara, fedha zinazotumika kujenga vyumba 8 vya madarasa, jengo la Utawala, majengo ya maabara, maktaba, chumba cha TEHAMA, matundu 16 ya vyoo pamoja na tanki kubwa la kuhifadhia maji lenye kujazwa lita elfu 10
#ArushaFursaLukuki
#KaziInaendelea
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa