Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wataalam wa Afya ya Binadamu na Mifugo kutumia miongozo mipya kutekeleza majukumu yao ili kuzuia tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa na kuepuka matumizi mabaya yasiyozingatia utaratibu kutoka kwa wataalam wa afya ya binadamu na wanyama.
Mhe. Ulega ametoa maagizo hayo wakati akifungua kongamano la tatu la kuzuia Usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, lililofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano Hoteli ya Mount Meru.
“Matumizi mabaya ya madawa yamesababisha ongezeko la vimelea vya magonjwa ambavyo havitibiki kwa urahisi kwa kutumia dawa zilizopo sokoni hali ambayo inasababisha vifo Zaidi ya laki saba kila mwaka”. Amesema Mhe. Ulega.
Naye Mkuu wa Mkoa Wa Arusha, Mhe. John V.K. Mongella, ametumia fursa hiyo kuomba Kongamano kama hilo kufanyika mara kwa mara katika ngazi za mikoa na Serikali za Mitaa ili elimu hiyo iweze kuwafikia wataalam wote na kupunguza changamoto hiyo.
“Sisi ndio tunakaa na hawa wananchi ambao ndio watumiaji wa dawa hizi na wahanga wa vimelea sugu kutokana na matumizi ya dawa, hivyo ni vyema viongozi wa ngazi za Mikoa na Wilaya kupata elimu hii kwa usahihi na kuipeleka kwa wananchi wengine kwenye ngazi zote”. Amesema Mongella.
Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya Mifugo Prof. Hezron Mnonga wakati akiwasilisha mkakati wa Serikali wa kuendeleza mapambano ya kuzuia usugu dhidi ya vimelea vya dawa, amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya mataifa yote duniani yanayotumia Mfumo wa Afya shirikishi unaolenga kupunguza changamoto hiyo.
“Nchi yetu tumebahatika kuanza kushughulikia hili tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa tangu mwanzi mwa mwaka 2011 na sasa malengo yetu katika kipindi hiki ni kushuka chini mpaka kwenye ngazi za vijiji na vitongoji tofauti ilivyokuwa kwenye mpango mkakati tulionao ambao ulijikita kwenye ngazi ya Taifa”.
Hata hivyo, kongamano hilo limeambatana na uzinduzi wa muongozo mpya kwa wataalam wa afya ya binadamu utakaowawezesha kutoa huduma za tiba kwa usahihi na kusaidia kupunguza changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa