Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amewakemia vikali wazazi wote ambao watoto wao wanapata Mimba wakiwa mashuleni kisha familia mbili zinakaa kusuluhisha kindugu kuacha mara moja tabia hiyo, badala yake kutoa taarifa sehemu husika ili hatua kali za kisheria zichuliwe.
Ameyasema hayo alipokuwa akiwakabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto 200 wanaotoka katika mazingira magumu na wengine yatima kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Amesema kwa kusuluhisha kindugu kunasababisha ongezeko la Mimba za utoto na kukatisha masomo na ndoto za watoto wengi wa kike.
Serikali inaendelea kukemia na kupiga vita mimba za utoto na kwamwe hatutafumbia macho wale wote watakaobainika kuwapa mimba watoto wa shule.
Aidha,Gambo amewataka wamiliki wa vituo vya makao ya watoto kufuata sharia zote za nchi na kuacha kuvitumia vituo hivyo kama njia ya kujipatia fedha na huku kiasi kidogo sana kikienda kwa watoto hao.
Pia, amewataka wamiliki hao kuzingatia maadili ya jamii yetu katika kuwalea watoto hao ili wakuwe kwenye mazingira ya maadili na tabia njema katika jamii yetu.
Ameipongeza benki ya Stanbic kwa kuona umuhimu wa kutoa bima hizo za afya kwa watoto 200 kwani wamewasaidia sana watoto hao hasa kwa kujali afya zao na amewataka wadau wengine kuiga mfano huo wa Stanbic benki, ili kulinda afya za watoto hao.
Mkuu wa Kitengo cha biashara Afrika kutoka benki ya Stanbic bwana Brayan Zwanzigira, amesema benki yao ipo pamoja kwa kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali ya maendeleo.
Amesema huduma hiyo watajitaidi kuendelea nayo kwa miaka kadhaa kadri watakavyoweza.
Nae Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha bwana Hargeney Chitukulo, amesema bado Mkoa wa Arusha una idadi ya watoto 54,000 wanaoishi kwenye mazingira magumu na kwa takwimu za kitaifa kwa mwaka 2017 hadi 2018 watoto 864,496 walibainika wanaishi kwenye mazingira magumu.
Amesema bado kuna changamoto kubwa ya ukatili wa kijinsia kwa watoto hasa katika mimba na ndoa za utoto katika jamii yetu.
Benki ya Stanbic imetoa kadi za bima ya afya inayojulikana kama toto afya kadi iliyoanzishwa na mfuko wa bima ya afya kwa lengo la kuwasaidia watoto kupata huduma za afya kwa bei ya shilingi 50,400 kwa mwaka.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa