Wananchi wa Kijiji cha Lemoot wametakiwa kuhakikisha Watoto wao wanapatiwa elimu hasa wasichana ili kuwasaidia ndoto zao walizo nazo ziweze kutimia.
Ameyasema hayo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta alipokuwa akikabidhiwa majengo ya shule ya msingi Lemoot iliyopo katika kata ya Lemoot wilayani Monduli.
Amesema wananchi hao wanatakiwa kuhakikisha Watoto wao wenye umri wa kwenda shule wanaenda ili kuondoa tatizo la utoro wa wanafunzi lakini pia elimu iwe ya mkazo kwa wasichana ili kuondoa mimba na ndoa za utoto.
Kimanta amesema, ili mtoto aweze kutimiza ndoto zao lazima wapiti shule kuwekewa misingi mizuri.
Mkurugenzi wa taasis isiyokuwa ya kiserikali ECLAT bwana Peter Tohima, amesema taasi yake imekuwa ikishirikiana na serikali kwa karibu sana kwa kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ya shule.
Aidha, kwa wilaya ya Monduli wameshakarabati jumla ya shule 5 ikiwemo shule ya msingi Lemoot ambayo jumla ya madarasa 4 yamekarabatiwa pamoja na ofisi ya walimu, majengo mawili ya vyoo yenye jumla ya matundu 16 kila moja yamejengwa na wametengeneza madawati 40.
Ukarabati huo na ujenzi umegharimu zaidi ya milioni 129 na majengo hayo yamekabidhiwa rasmi kwa serikali ili kuyaendeleza katika kusaidia kutoa elimu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa