Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amepongeza jitihada za taasisi zote za sekta ya fedha nchini kuhimili vihatarishi vyote vilivyojitokeza na kufanya sekta hiyo kuwa imara na himilivu kwa kuongeza ubunifu na uwezo wa kubadilika kuendana na mazingira yaliyopo.
Amesema hayo wakati akifungua Kongamano la 21 la Taasisi za Fedha linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha tarehe 7 Machi 2024 likiwa na mada kuu isemayo: "Kuimarisha Ustahimilivu wa Sekta ya Fedha Nyakati za Changamoto za Kiuchumi".
“Hakika, mmesaidia kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi na maendeleo,” Dkt. Mpango amewaeleza viongozi wa taasisi za fedha ambao
Aidha, Makamu wa Rais amewataka watoa huduma wa mifumo ya malipo kuendelea na ubunifu ili kudumisha utengenezaji wa bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya jamii yetu kuendana na mahitaji yake yanavyobadilika.
Amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya malipo kwa njia za kidigitali, hasa katika sekta za benki, bima, mifuko ya Hifadhi ya Jamii na huduma nyingine.
“Mabadiliko haya yanapelekea uhitaji wa kuhama kutoka kwenye matumizi ya pesa taslimu kwenda kwenye njia za malipo za kielektroniki ili kupunguza hatari zinazohusiana na kutumia pesa taslimu na kuongeza urahisi wa ufanyaji malipo,” amesema.
Dkt. Mpango ameipongeza Benki Kuu na taasisi zote zilizoshiriki katika uundwaji wa Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Hapo, yaani Tanzania Instant Payment System (TIPS).
“Ninatarajia kwamba mfumo wa TIPS utasaidia kuendeleza huduma rasmi za kifedha na kupunguza gharama za miamala,” amesema Makamu wa Rais ambaye baadaye alizindua rasmi mfumo wa TIPS.
Aidha, ameipongeza Benki Kuu kwa kuanza kutumia mfumo mpya wa utekelezaji wa sera ya fedha unaotumia riba, akieleza matumaini kwamba utaimarisha ufanisi wa sera ya fedha katika mazingira ya sasa ya kiuchumi na hivyo kutoa ishara kwa riba za mikopo inazotolewa na taasisi za fedha ili kuchochea uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Chanzo: BOT
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.