Wananchi wa Mkoa wa Arusha wametakiwa kulima mazao yanayostawi kwa muda mfupi na kutunza maji pindi mvua zitakaponyesha.
Yamesemwa haya na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa akifungua kikao cha ushauri cha Mkoa (RCC) mapema leo hii.
Amesema, kwa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) mvua zitakuwa za wastani kwa baadhi ya maeneo na chini ya wastani kwa maeneo mengine, hivyo wananchi wa Arusha waendelee kuyaelewa mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Uchumi na uzalishaji bwana Daniel Loiruck amewahasa wafugaji kutunza baadhi ya malisho kwa kutumia matumizi bora ya ardhi ili yaweze kusaidia katika kipindi cha ukame.
Amesema pia, Mkoa unaendelea kuelimisha wafugaji kuvuna mifugo yao kabla ya kiangazi kikali ili kuepuka kupata hasara kwa mifugo yao kufa au kuwa na uzito mdogo na kukosa bei katika soko.
Kikao cha ushauri cha Mkoa kimefanyika cha kwanza katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 kikiwa kimejumuisha wataalamu wa Mkoa, halmashauri na taasisi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mkoa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.