Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter Van Acker, ametembelea miradi ya ushirikiano kwenye Sekta ya kilimo inayofadhiliwa na Serikali ya Ubeligii inayotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la rikolto mkoani Arusha
Balozi Acker amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kusimamia miradi hiyo kwa uaminifu ili kusaidia wakulima wa Tanzania katika kuboresha afya na kuinua kipato cha wananchi na Serikali kwa ujumla.
Aidha ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea mashamba ya wakulima wanaonufaika na miradi hiyo yalipo kata za Nduruma na Mbuguni, Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.
“Nimefurahi sana kutembelea miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Nchi yangu Mkoani Arusha,kwa niaba ya Serikali ya Nchi yangu tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia wakulima na ninatamani kuona miradi kama hii ikifanyika kwenye maeneo mengine Nchini”. Amesema Balozi Van Acker.
Hata hivyo, Balozi Acker ameelezea furaha yake kuhusu maendeleo yanayopatikana kupitia ushirikiano huu, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za pamoja za kuboresha kilimo na kukuza uchumi wa vijijini.
Kwa upande wake Mratibu wa programu wa Shirika hilo la Rikolto amesema kuwa l;engo kuu la Shirika hilo ni kuongeza uzalishaji, kuboresha mifumo ya kilimo, na kusaidia wakulima kupata fursa za masoko ambapo Miradi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wakulima na jamii za vijijini.
Vile vile, wakulima hao wameweka wazi jinsi shirika hilo lisilo la kiserikali linavyowasaidia katika kutoa elimu na kuwawezesha katika kuzalisha mazao yenye ubora katika masoko ya nje na ndani ya nchi sambamba na kuwaunganisha na wanunuzi wa mazao hayo katika maeneo tofauti tofauti.
Awali, Miradi ya ushirikiano wa kilimo inayofadhiliwa na Ubelgiji inasaidia wakulima wa Tanzania kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa