"Ujenzi wa Barabara ya Mianzini hadi Ngaramtoni yenye urefu wa kilomita 18 itafungua fursa mbalimbali za maendeleo ikiwemo kurahisisha usafiri kwa wananchi".
Yamesemwa hayo na Makamu wa Raisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango baada ya kuweka jiwe la msingi katika barabara hiyo eneo la Ngaramtoni ya juu.
Amesema,Serikali imewekeza fedha nyingi katika miundombinu ya barabara ili kuwarahisishia wananchi katika shughuli zao za kiuchumi.
Pia, Dkt. Mpango amewataka askari wa usalama barabara kuisadia serikali kusimamia sheria za usalama barabarani kihalali ili kupunguza vifo vya watu na hata wengine kuachwa wakiwa walemavu wa viungo.
Vilevile, amewahasa madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani, ili waweze kulinda uhai wao.
Dkt. Mpango amesema juhudi za serikali zilizofanywa hadi sasa katika bajeti ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilikuwa bilioni 275 mwaka 2022/2023 ilikuwa bilioni 771.8 na bajeti tarajiwa ya 2023/2024 inakadiriwa kuwa bilioni 818.02.
Amesisitiza juhudi hizo ni kuwawezesha TARURA kuhudumia vizuri mtandao wa barabara kwa ukubwa.
Kwa Mkoa wa Arusha, TARURA wamepatiwa bilioni 19.5 kwa bajeti ya mwaka 2023/2024 na hii itasadia kurekebisha zaidi barabara zote hata zile zilizoharibiwa na mvua.
Aidha, amewataka wananchi wakatunze mazingira kwa kuacha kukata miti hivyo na kuwataka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kupanda miti ya vivuli na Matunda katika barabara hiyo ili iweze kupendeza zaidi.
Akisoma taarifa kwa ufupi, Naibu Waziri wa ujenzi na miundombinu Godfrey Kasekenya amesema fidia ambayo itatolewa ni kwa wale wananchi wa barabara kuanzia Olemringaringa hadi Ngaramtoni na wale wananchi wa Mianzini hadi Ngaramtoni hawatalipwa kutokana na kanuni na sheria za barabara.
Nae, Mtendaji wa TANROADS Mhandisi Logatius Matibila amesema barabara hiyo ya kilometa 18 itagharimu bilioni 22.2 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT) hadi kukamilika kwake.
Amesema mkataba wakuanza ujenzi ulisainiwa Januari 19, 2022 na ujenzi ulianza Mei 20,2022 na unatarajiwa kukamilika Agosti 2023.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya Barabara na kuwezesha Mkoa kuendelea kuboresha barabara zake ili ziwe rahisi kupitika.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango amemaliza ziara yake ya kikazo ya siku 4 kwa Mkoa wa Arusha na ameridhishwa na miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa katika Mkoa wa Arusha hususani aliyoipitia na kuwataka wananchi waitunze kwani fedha nyingi zimetumika kuijenga ambazo ni kadi zao.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa