Na Elinipa Lupembe
Mradi wa Kuboresha upatikanaji wa Fursa sawa katika Ujifunzaji Bora kwa elimu ya awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST), umewezesha, ongezeko la idadi ya wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la awali na darasa la kwanza shule mpya ya msingi Emayan, kijiji cha Lemanda Kata ya Oldonyosambu, wilaya ya Arumeru, iliyojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 348.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo mpya, Mwl. Moi Msilu, amethibitisha kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza inayofikia wanafunzi 373 walioandikishwa kuanza shule mwaka mwaka wa masomo ulioanza rasmi Januari 08, 2024.
Amesema kuwa, uwepo wa shule katika kijiji cha Lemanda, umeongeza hamasa kwa wazazi kuwaandikisha watoto kuanza shule, tofauti na miaka ya nyuma wazazi waliwachelesha watoto kuanza shule kutokana na umbali iliyowalazimu kwenda shule ya Msingi Oldonyosambu, ambako mtoto alilazimika kutembea Km 6 mpaka 8 kwenda na kurudi shuleni kila siku.
"Kwa sasa shule ina jumla ya wanafunzi 668 kati ya hao, wanafunzi 373 ni wa darasa la awali na la kwanza sawa na asilimia 56 huku darasa la pili mpaka la saba wakiwa 295 sawa na asilimia 44, utagundua uandikishwaji umeongezeka sana kutokana na mwamko wa wazazi uliosukumwa na shule kuwa jirani nao" Ameweka wazi Mwl. Msilu
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Lemanda Mhe. Mosses Ngalima, amesema kuwa, uwepo wa shule karibu, umewapa fursa watoto wengi kupata elimu, tofauti na hapo awali licha ya wazazi kushindwa kuwaandikisha watoto shule kwa wakati, wapo watoto walizembea kufika shule kwa kujificha na kusababisha utoro na wapo walioacha shule, kutoka na umbali wa mahali shule ilipokuwa.
"Uwepo shule kijijini hapa, umewapunguzia watoto mwendo, hakuna mtoto anayetembea zaidi ya Km mbili kwenda na kurudi shuleni, watoto wanasoma vizuri na asilimia kubwa wanafika shule kwa wakati, tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hasaan kwa kutujali sisi jamii yawafugaji, jamii imehamasika kila mzazi sasa anamruhusu mtoto wake kwenda shule kwa amani" Amesema Mhe.
Ameongeza kuwa, wanaamini Serikali imetumia fedha nyingi sana kutekeleza mradi huo, lakini kipekee wananchi wa Lemanda wamenufaika sana, watoto wao wamepata fursa ya kupataelimu, fursa ambayo baadhi ya watoto waliikosa kwa kupelekwa kuchunga ng'ombe na wengine kuozeshwa katika umri mdogo.
Hata hivyo wanafunzi wa shuleni hapo wameishukuru Serikali kwa kujenga shule kijiji kwao na kumuahidi Mhe. Rais Mama Samia, kusoma kwa bidii mpaka vyuo vikuu na hatimaye kuzifikia ndoto zao za kitaaluma.
Obadia Philipo darasa la V, mwenye ndoto ya kuwa Daktari, amemshukuru Mama Samia, na kumuahidi kusoma kwa bidii kwa kuwa shule ina majengo mazuri ya kisasa, walimu wanawafundisha vizuri.
"Tunamshukuru mama Samia, kwa kutujengea shule ambayo imasababisha sisi wasichana wa kimaasai kupata nafasi ya kusoma, tunamuombea Mwenyenzi Mungu aishi maisha marefu"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa