Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dkt. Fredrick Shoo amesema Kanisa hilo nchini Tanzania litaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita katika kupiga vita wanaokanyaga na kuminya haki za watu pamoja na kupambana na imani za kishirikina nchini Tanzania kwani Imani hizo zimesababisha watu wengi kutopea kwenye umaskini.
Dkt. Shoo ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 29, 2024 kwenye Ibada maalum ya kumstaafisha Kwa Heshima Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt. Solomon Massangwa, wakati akitia msisitizo kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda aliyetaka Jamii kuachana na imani potofu na kushabikia mambo yanayowachelewesha katika maendeleo.
"Tunaona mambo mengi na balaa nyingi zimekuja katika nchi hii kwasababu wapo hata Viongozi wa ngazi za juu sana wanashiriki katika mambo hayo kwasababu ya imani zao kuwatuma wakati wa kutafuta vyeo nk, ni wajibu wetu wa Viongozi wa dini kushirikiana na viongozi wa serikali kukemea mambo hayo." Amesema Dkt. Shoo.
Awali Mkuu wa Mkoa amewaambia washirika wa Kanisa la KKKT Kimandolu kuwa unyang'anyi wa haki umekithiri kwenye jamii, akilitaka kanisa kusimama katika misingi yake katika kuilinda Haki ya kiraia pamoja na kupambana na imani za kishirikina hasa wakati huu wa kuelekea kwenye chaguzi mbalimbali za kisiasa akiamini kuwa kusimama imara kwa Kanisa ni msingi wa upatikanaji wa haki kwa wote.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa