Katika hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Halmashauri ya Wilaya ya Longido imeandaa mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa uandikishaji wa ngazi ya kata. Mafunzo hayo, yamefanyika leo tarehe 4 na kumalizika 5 Desemba 2024 katika ukumbi wa Halmashauri, yalilenga kuimarisha mchakato wa uandikishaji wa wapiga kura wapya, kuboresha taarifa zilizopo, na kufuta majina ya wale waliopoteza sifa za kupiga kura.
Mafunzo hayo yaliwaleta pamoja maafisa wa kata kutoka kata zote 18 za Longido. Wakizungumza katika uzinduzi wa mafunzo hayo, viongozi wa uchaguzi waliweka wazi umuhimu wa zoezi hilo kwa mustakabali wa demokrasia na uwakilishi wa wananchi.
Akifungua mafunzo hayo, Msimamizi wa Uandikishaji wa Jimbo, Bw. Nevilling Lymo, aliwahimiza washiriki kuwa makini na weledi. “Zoezi hili si tu jukumu la kawaida; ni dhamana kubwa kwa taifa. Tunatarajia mtumie maarifa haya kuandikisha kila mwenye sifa, kuboresha taarifa sahihi, na kuhakikisha wale wasiostahili hawabaki kwenye daftari,” alisema.
Aliongeza kuwa ushirikiano baina ya wasimamizi wa kata na wasaidizi wao ni muhimu katika kufanikisha uandikishaji wa wapiga kura wenye sifa ili kuhakikisha usawa na haki katika uchaguzi ujao.
Afisa Uchaguzi wa Wilaya, Bw. Manase Msechu, naye aliwataka washiriki kuwa na utulivu na makini katika kufuatilia kila somo. “Hili ni zoezi nyeti linalohitaji umakini mkubwa. Kuboresha daftari kunatoa fursa kwa kila raia mwenye sifa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi. Hakikisheni kila taarifa mnaijadili kwa kina na kwa usahihi,” alisisitiza.
Washiriki wa mafunzo hayo walionekana kufurahia mafunzo hayo, wakieleza kuwa yamewapa mwongozo bora wa namna ya kusimamia mchakato wa uandikishaji kwa ufanisi. Mafunzo hayo yameacha matumaini makubwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 utakuwa wa haki na unaoaminika kwa pande zote.
Zoezi hili linachukuliwa kama hatua muhimu ya kuimarisha demokrasia na kuwapa wananchi wa Longido fursa ya kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa