Daktari wa Watoto Hospitali ya Jeshi kanda ya Arusha, hospitali ya Jeshi Monduli Meja Dkt. Emmanuel Luchagula amesema kuwa, katika kambi ya Madaktari Bingwa na Mabingwa Wabobezi Arusha, iliyofanyika kwa siku 7 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jumla ya watoto 4,616 wamehudumiwa na kupatiwa matibabu, vipimo, dawa na vifaa tiba.
Meja Dkt. Luchangula amesema kuwa, katika idadi hiyo, watoto wengi wamekutwa na changamoto ya mfumo wa hewa, pumu ya ngozi na macho huku kundi dogo likiwa na changamoto ya mtindio wa ubongo unaotokana na uzazi pingamizi, magonjwa ambayo yanasababishwa na mifumo ya maisha na yanaweza kuepukika.
Amesema kuwa, takwimu hizo zinaonesha changamoto za kiafya ni nyingi kwa jamii, zinazotoa funzo kwa wahudumu wa afya kujitathmini na kuitathmini mifumo ya utoaji huduma za afya kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kuzuia kupata magonjwa ambayo si ya lazima husuani magonjwa yasiyoambukiza.
"Mkuu wa mkoa ametupa 'challenge' watoa huduma za fay, ambapo kila siku madaktari tunatibu lakini tunajiuliza wagonjwa hawa wametoka wapi? Ni kama vile Mhe. Makonda ametupa jiwe gizani ambalo imetupa picha ya kutambua hali halisi ya namna wananchi wetu wanasumbuliwa na magonjwa huku wakishindwa kumudu gharama za matibabu " Ameweka wazi Dkt.
Aidha ametoa wito kwa madaktari na wahudumu wa afya kila mmoja kutumia nafasi yake katika kutatua changamoto za wagonjwa huku akisisitiza Kitengo cha Kinga Tiba, kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji wa afya pamoja na matumizi mabaya ya dawa bila ushauri wa daktari hususani matumizi ya dawa aina ya 'antibiotic' ambayo ina madhara makubwa hususani kwa watoto.
"Wapo wazazi wenye tabia ya kuwapa dawa watoto bila ushauri wa daktrai matokeo yake zinatengeneza sumu na usugu kwa watoto, wapo wazazi wanaowaachisha watoto kunyonya katika umri mdogo jambo linalosababisha watoto kupata 'allergy' ya maziwa ya ng'ombe na maziwa 'artificial', jambo linalosababisha magonjwa ya pumu ya ngozi na macho" Amesema Dkt. Luchangula.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa