Na Elinipa Lupembe
Jamii imesisitizwa kuzingatia umuhimu wa lishe bora kwa vijana wa rika balehe la miaka 10 -19 ambayo ni hatua muhimu ya ukuaji mara baada ya siku 1000 za mwanzo za maisha ya mtoto.
Rai hiyo imetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Lishe Mkoa Mkoa wa Arusha mwaka 2023, yaliyofanyika kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Meru, wilaya ya Arumeru.
Akizungumza kwa niaba Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John VK. Mongella, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Charles Rashid Mkombachepa,amesema kuwa suala la Lishe ni la muhimu katika afya ya binadamu lakini umuhimu unajikita zaidi kwenye hatua za makuzi ikiwemo hatua za makuzi kwa vijana wa rika balehe.
Amesema kuwa jamii inaoaswa kuzingatia lishe bora kwa vijana , kwa kuwa hatua ya ukuaji kwa vijana wa rika balehe, ndio maandalizi ya maendeleo ya mwili katika uzazi lakini maendeleo katika maandalizi ya nguvu kazi kwa maenedeleo ya kijamii na kiuchumi.
"Lishe bora kwa vijana balehe ni muhimu kwa kipindi cha miaka 10 -19 ndio fursa adhimu ya ukuaji na maendeleo ya binadamu baada ya siku elfu moja za mwanzo wa maisha ya mtoto, hatua ambayo inamuandaa kijana kuwa nguvu kazi ya Taifa." Alisema Mkombachepa.
Aidha, ameeleza kuwa vijana balehe wana umuhimu wa kuzingatia lishe kwani ndio msingi wa maendeleo ya binadamu na ya Nchi, hivyo jamii kwa ujumla wake wanapaswa kuzingatia na kichukua hatua stahiki kuhakikisha vinaja wanapata lishe bora kwa afya zao.
Naye Mkuu wa Idara ya ya Afya Halmashauri ya Meru, Dkt. Evarist Chiweka, ameeleza kuwa Afya bora kwa vijana ni muhimu kwa kuwa ndio msingi wa nguvu kazi ya jamii na Taifa.
Aidha ameyataja madhara ya utapiamlo kwa wanawake na watoto wadogo ambao ndio wahanga wakubwa, unasababisha vifo kwa watoto wakati wa kujifungua, kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu na watoto ambao hawajafikisha muda wake(Njiti).
Naye Afisa Lishe Mkoa wa Arusha Dotto Milembe ameeleza dhumuni la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa katika jamii, kuhusu afya yanlishe na umuhimu wa lishe bora wa vijana hususani vijana wa rika balehe ambao ndio msingi wa nguvu kazi ya jamii na Taifa.
Ameyataja makadirio ya kidunia yanaonyesha kuna vijana Milion 1.2 wenye umri wa miaka 10-19 ambayo inaongezeka kwa kasi kubwa huku Tanzania ikikadiriwa kuwa robo ya watu wote ni vijana wa rika balehe.
Amesisitiza kuwa huduma za Afya ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Nchi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Sura ya 3 Ibara ya 81.
Iren Clement Makundi ni mwanafunzi kutoka chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, amefurahi kushiriki katika maadhimisho hayo kwani amejifunza umuhimu wa lishe bora kwa vijana balehe.
" Nimeokolewa na elimu finyu iliyokuwepo katika kichwa changu kwani leo nimeelewa umuhimu wa lishe bora kwa kijana hasa wakati wa kupevuka" Alisema Iren.
Awali maadhimisho hayo mkoa wa Arusha, yameambatana na utoaji wa huduma bure za Afya, ikiwemo upimaji wa hali ya lishe, ulinganisho wa Urefu na Uzito pamoja na kutoa elimu ya vyakula ya Afya na lishe yakiwa yamebeba Kauli Mbiu ya " Lishe bora kwa Vijana balehe ni chachu ya mafanikio yao"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa