Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha, imetembelea na kukagua hali ya mradi wa ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana shule ya sekondari Mringa, mabweni yaliyojengwa kwa gharala ya shilingi milioni 260, fedha kutoka Serikali Kuu kupitia miradi ya kuboresha miundombinu ya Sekondari Nchini (SEQUIP).
Wajumbe hao wameridhishwa na kupongeza utekelezaji wa mradi huo, ambao umeongeza ari ya watoto wa kike kusoma kwenye mazingira salama chini ya uangalizi wa walimu muda wote, amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), kurekebisha mfumo wa maji shuleni hapo na kuhakikisha maji yanatoka shuleni hapo muda wote.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Loy Thomas Ole Sabaya, amewapongeza wananchi kwa usimamizi wa mradi huo wa mabweni pamoja na kuwaagiza AUWSA, kushughulikia tatizo la maji shuleni hapo, ili kuwe na maji ya uhakikika shuleni hapo.
"Shughulikieni tatizo la maji shuleni hapa, maji yatoke siku zote, hapa kuna wanafunzi wengi hivyo uwepo wa maji ya uhakika ni muhimu, ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na wanafunzi kutumia muda mwingi kusoma badala ya kwenda kutafuta maji na ndoo kichwani".Amesema Mwenyekiti Sabaya
Hata hivyo, ameipongeza Serikali kupitia halmashauri kwa mradi huo mzuri, uliotekelezwa kwa ubora wa viwango vinavyoendana na thamani ya pesa iliyotolewa na Serikali na kuwasisitiza wazazi na kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule pamoja na kuwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii.
"Niwasihi wanafunzi kusoma kwa bidii na kufikia ndoto zenu, Serikali imeshawaandalia miundombinu na mazingira rafiki na salama ya kujisomea hakikisheni mnasoma kwa bidii na kupata ujuzi utakaokuja kulitumikia taifa lenu hapo baadaye" Amesema Sabaya
Awali, Wajumbe wa Kamati hiyo, wanafanya ziara ya kawaida ya siku mbili ya kutembelea na kukagua miradi ya Maendeleo, ikiwa ni ukagua wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM katika halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa