Na Elinipa Lupembe.
Kongamano la kwanza la Wanamipango nchini mwaka 2023, linafanyia mkoani Arusha, mara baada ya Serikali ya awamu ya Sita, kurejesha Wizara ya Mipango na Uwekezaji, chini ya Ofisi ya Rais, na kufunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (MB), kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K.Mongella ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kurejesha, Tume ya Mipango na Uwekezaji huku Kongamano la kwanza la Wanamipango nchini likifanyika Mkoani Arusha na kuipongeza, Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa kuchagua Mkoa wa huo kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo.
Mhe. Mongella amekiri kutambua umuhimu wa kupanga kuanzia ngazi ya mtu binafsi, familia, Taasisi hadi Taifa, mipango inayowezesha kutoa huduma, kulingana na uhitaji ili kuleta maendeleo na kuongeza kuwa, amekuwa akiwasisitiza wataalam wa Mkoa na ngazi zote za Arusha, kuhakikisha wanakuwa na mipango ya pamoja inayotekelezeka ili kuleta maendeleo kwenye jamii zinazohudumiwa.
"Binafsi ninaamini kushindwa kupanga ni kupanga kufeli, kwa kuzingatia hili, kila Mwana mipango analo jukumu la kuimarisha mipango inayozingatia mahitaji ya jamii na rasilimali zilizopo"
Aidha, ameutaja umuhimu wa Kongamano hilo, likiwa limekusanya Wataalam na Wadau wa mipango kutoka sehemu mbali mbali za nchini, wakiwa na lengo la kujengeana uwezo na kutengeneza mfumo mzuri wa upangaji kwa maendeleo ya Taifa letu.
Aidha ametumia fursa hiyo, kuwakaribisha Wanamipango mkoani Arusha, mkoa ambao ni kitovu cha Utalii na kuwataka, washiriki kutembelea vivutio vya utalii ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais za kukuza utalii nchini na kuwahakikishia usalama wa washiriki wote kwa kipindi chote watakapo kuwa mkoani hapo.
"Kwa niaba ya wananchi wa Arusha, na Uongozi wa Mkoa, tupo tayari kutoa ushirikiano muda wote tutakapohitajika, ninawasihi washiriki mpatapo nafasi msisite kutembea kujionea mandhari nzuri ya Mkoa wetu" Amesema Mhe. Mongella.
Kongamano la Wanamipango mwaka 2023, limefunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (MB), linalofanyika kwa siku 4, kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), lenye Kauli Mbiu ya "Fikra za Pamoja na Utekelezaji, Ulioratibiwa kwa Ustawi Jumuishi"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa