Na Elinipa Lupembe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa jengo jipya la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha Parokia ya Karoli Lwanga eneo la Usa- River, wilaya ya Arumeru
Akizungumza wakati wa kukabidhi sadaka hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, ambaye amemuwakilisha Mheshimiwa Rais kwenye Harambee hiyo, amesema kuwa, Mhe. Rais amemuagiza kuwasilisha sadaka yake, yeye na familia yake ya shilingi milioni 100.
Mhe. Makonda ameweka wazi kuwa, licha ya sadaka hiyo, Dkt. Samia amemuagiza kufikisha salamu zake za upendo, zinazokwenda kufanikisha ujenzi wa nyumba ya Bwana, Sadaka ambayo ameiombea ikadumishe Umoja na Mshikamano ndani ya Kanisa na Taifa kwa ujumla wake.
"Ninaamini waumini hawa wameweka nia moja ya kumjengea Mungu Kanisa, naungana na waumini wa Parokia ya Karoli Lwanga, kutimiza dhamira yao katika kumtumikia Mwenyenzi Mungu, sadaka hii ikasimame katika upatanishi na kujenga umoja wa Kanisa na Taifa letu la Tanzania" Mhe. Makonda amenukuu salam za Dkt. Samia Suluhu Hassan @samia_suluhu_hassan
Hata hivyo, Mhe Makanda ametoa Mchango wa shilingi Milioni 10, na kuiombea sadaka yake, ikanene mema na kuwa baraka kwa wakazi wote wa Arusha kwa kuondoa mapooza pamoja na kuitakasa ardhi Arusha dhidi ya ajali zote zinazoondoa uhai wa watu wengi hasa watoto wadogo wenye ndoto za kutimiza.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuuombea uzao wa wanaarusha kuwa wenye baraka huku akihimiza wakazi wote na kumtanguliza Mungu na kuwa na hofu ya Mungu katika maisha yao ya kila siku, ili kuendelea kuneemeka na baraka zake.
Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga ilianzishwa mwaka 1975 na kujengwa kanisa lililokuwa na uwezo wa kubeba waumini 600 kwa wakati mmoja na kulingana na wingi wa waumini kwasasa, Kanisa hilo limeamua kujenga kanisa jipya litakalokuwa na uwezo wa kubeba waumini 2500 kwa wakati mmoja.
Awali, Jengo jipya linakadiriwa kutumia shilingi Bilioni 2.7 ulianza mwaka 2010 umefikia 54% ukigharimu bilioni 1.4 na kusalia Bilioni 1.3.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa