Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania Dkt. Godwin Mollel amesema wakuu wa mikoa wana mambo mengi ya kujifunza kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kutokana na namna ambavyo amekuwa akifanikiwa kwenye programu mbalimbali za kuhudumia wananchi na kutekeleza maelezo ya serikali kuu kikamilifu.
Naibu Waziri wa afya ametoa kauli hiyo siku ya Jumamosi Juni 29, 2024 alipotembelea kambi ya madaktari bingwa inayoendelea Mkoani Arusha kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid, akifurahishwa na uratibu wa Kambi hiyo pamoja na wingi wa watu waliopata matibabu kwenye kambi hiyo inayotarajiwa kumalizika Jumatatu ya wiki ijayo.
"Nikuambie tu Mhe. Mkuu wa mkoa tunakuelewa sana na watanzania wanakuelewa sana na nikuambie tu wewe simama kwasababu wewe ni Daud wala usiogope na umeshika kombeo na usiogope mishale mingi huwa inaendaga pale patakatifu kwasababu shetani huwa anapachukia."
Aidha Dkt.Mollel amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuzifanya vyema kazi zote za Rais Samia zinazokuja Mkoani Arusha, akimtaka kutokatishwa tamaa katika kuwatumikia wananchi kutokana na ukosoaji na maneno mabaya yanayoelekezwa kwake.
Katika hatua nyingine Naibu waziri huyo wa afya ametangaza kuwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza siku moja ya Kambi hiyo ya Matibabu ya kibingwa na hivyo kutakiwa kuisha Jumatatu ya wiki ijayo tofauti na ilivyokuwa imepangwa awali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa