Mafundi simu wametakiwa kuwa waaminifu kwa wateja wao pindi wanapowatengenezea simu zao.
Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Iddi Kimanta alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya mafundi simu wa Kanda ya Kaskazini ilijumuisha mikoa ya Arusha,Tanga,Manyara na Kilimanjaro,yaliyofanyika Mkoani Arusha.
Amesema serikali inatambua uwepo wao ndio maana mafunzo hayo yakatolewa kwao kupitia Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na chuo cha ufundi VETA.
Hii yote nikuwajengea uwezo mafundi simu nchini ili kazi zao ziwe bora na zinazotambulika katika jamii zao.
Aidha, Kimanta amewataka kutumia vikundi walivyonavyo kwa kila mkoa kwa ajili ya kuombea mikopo katika taasis mbalimbali za fedha na pia kujipatia bima za afya kwani fursa hizo zitawasaidia katika kukuza biashara zao.
Mkurugenzi wa chuo cha ufundi VETA bwana Patrace Bajulu amesema,jumla ya mafundi 417 ndio walioomba kupatiwa mafunzi hayo kutoka kanda ya Kaskazini lakini waliopata nafasi ni 200 na wengine 217 wamekosa kutokana na bajeti kutotosha.
Amesema bado serikali inaendelea kutafuta namna ya kuhakikisha mafundi wote wanapatiwa mafunzo hayo.
Bwana Bajulu amewataka mafundi hao kutumia fursa hiyo ya mafunzo ili kujipanua katika soko.
Mafunzo kwa mafundi simu yalianza mapema mwaka huu Mkoani Dodoma na kuendelea kutolewa katika kanda mbalimbali hapa nchini.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa