Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema limejipanga vyema kuhakikisha kuwa sikukuu ya kufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025 inasherehekewa kwa amani na utulivu hasa kwa kuzingatia kuwa kutakuwa na mkesha wa siku tatu katika Jiji la Arusha.
Leo Disemba 30, 2024, akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amewaambia wanahabari kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameandaa mkesha wa siku tatu kuanzia Disemba 29 hadi 31, 2024 na kubainisha kuwa baadhi ya barabara zitafungwa ili kufanikisha shamrashamra hizo.
Kamanda wa Masejo amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama litahakikisha maeneo yote yanakuwa na ulinzi wa Askari ambao watakuwa katika doria za miguu, pikipiki, na magari katika kila kona ya Jiji na wilaya zote za Mkoa huo.
Aidha Jeshi la Polisi mkoani Arusha limepiga marufuku wananchi kuchoma matairi, kupanga mawe barabarani pia Wamiliki wa bar na kumbi za starehe wametakiwa ku,ingatia masharti ya leseni zao ambazo zinaonesha muda halisi wa kufunga na kuepuka kujaza watu kupita kiasi.
Sambamba na hilo kamanda wa Polisi amesisitiza kuwa Kwa upande wa upigaji wa fataki, watakaoruhusiwa ni wale tu ambao watakaokuwa na vibali na hawataruhusiwa kufyatua katika makazi ya watu akikumbusha wananchi pia kutokuacha nyumba zao bila ya uangalizi pindi wanapokwenda kwenye sherehe sikukuu hiyo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa