katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Albano Musa amewataka wajumbe wa kikao cha lishe ngazi ya Mkoa, kufanya utekelezaji wa kuanzisha bustani pamoja na vilabu vya lishe kwenye shule zote za Mkoa huo ili kukabiliana na changamoto za lishe kwa watoto.
Ameyasema hayo wakati wa kikao cha kamati ya lishe Mkoa wa Arusha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25 kilichofanyika leo 07 januari, 2024 kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Katibu Tawala huyo, amesema kuwa kiashiria hicho kiwe kimepata mafanikio makubwa sana kwa asilimia mia moja katika kikao kitakachofuata na kama kutakuwa na changamoto yoyote ya kutoanzisha bustani na vilabu vya lishe iwasilishwe mapema ili kuchukua hatua.
Hata hivyo, amemtaka Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Sara Mlaki kufanya ufuatiliaji kwa wasambazaji wa unga na bidhaa mbalimbali zisizo na virutubisho shuleni kuwekewa marufuku.
Kwa upande wake Afisa lishe Mkoa wa Arusha, Dotto Milembe amesema kuwa, kupitia viashiria vinavyosimamiwa na mkataba wa Lishe, Mkoa umefanya vizuri kwa zaidi ya asilimia 90 licha ya kuwepo changamoto kwenye viashiria vitatu ikiwemo hiyo ya uanzishwaji wa bustani na vilabu vya Lishe.
Awali, Mkoa wa Arusha kwasasa unakabiliwa na changamoto ya ongezeko la watoto kuzaliwa na uzito mdogo pamoja na upungufu wa damu kwa akinamama huku mikakati ikiendelea ili kupunguza changamoto hiyo ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu lishe bora.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.