Wafugaji wa Mkoa wa Arusha wametakiwa kuchangamkia soko la uuzaji wa mifugo yao katika kiwanda cha nyama cha Eliya Food kilichopo wilayani Longido.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Kimanta alipotembelea kiwanda hicho na kujionea namna kinavyofanya kazi za uzalishaji wa nyama.
“Kwanini wafugaji wetu wakauze mifigo yao nchi za jirani wakati tayari tuna mwekezaji hapa ambae yupo tayari kununua mifugo takribani 1000 kwa siku?”.
Amesema wawekezaji wazalendo kama hao wanatakiwa kuungwa mkono kwa juhudi kwani wangeweza kwenda kuwekeza Mkoa mwingine wowote lakini wao wakachagua Mkoa wa Arusha wakiwa na lengo la kuwatafutia masoko ya mifugo wafugaji.
Aidha, Kimanta amewashauri watafute mawakala wakutosha wa kuwakusanyia mifugo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili waweze kupata mifigo ya kutosha katika uwendeshaji wa kiwanda chao.
Amesisitiza kuwa, serikali itashirikiana na uongozi wa kiwanda hicho na kuhakikisha kinakuwa na kutengeneza soko kubwa ndani na nje ya nchi, kukuza uchumi wa Mkoa na kutengeneza ajira za kutosha kwa wana Longido.
Nae, Mkurugenzi wa Kiwanda bwana Shabia Virgi amesema, malengo ya kiwanda chao ni kuhakikisha nyama ya Tanzania inauzika hadi nchi za nje na kuifanya nchi itambulike zaidi.
Bwana virgi amesema mpaka sasa wamesha chinja mbuzi 1400 ikiwa ni hatu ya majaribio na kiwanda kinauwezo wa kuchinja mbuzi 1000 kwa siku.
Amesema changamoto kubwa waliyonayo ni upatikanaji wa mifugo kwa bei ya juu kutoka kwa wafugaji ambayo umepelekea kiwanda kuchinja nyama kwa kiwango kidogo mbuzi 600 kwa siku badala ya 1000 kwa siku.
Mhe. Kimanta amefanya ziara ya kutembelea kiwanda cha Eliya Food oversees kilichopo wilayani Longido ikiwa ni moja ya utaratibu wake wa kutatua changamoto mbalimbali kwa wawekezaji waliopo katika Mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa