Watendaji wa serikali katika ngazi za vijiji na kata wametakiwa kuwa na madaftari yenye orodha ya majina ya wananchi wao,hii itawasaidia kuwafahamu na kujua changamoto zao.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta alipokuwa akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia katika Jeshi la Polisi Mkoani Arusha.
“Kila kiongozi anatakiwa kuwafahamu wananchi wake na changamoto zao huku akizitatua kadri ya uwezo wake,hii itasaidia kupunguza ukatili wa kijinsia katika maeneo yao”.
Amesema itakapotokea kesi ya ukatili wa kijinsia katika eneo la kiongozi yoyote na yeye yupo na hajachukua hatua zozote basi atatakiwa kujielezea.
Hivyo, amewataka viongozi hao wakatekeleze majukumu yao ikiwemo kutatua changamoto za wananchi wao hasa zinazohusu usalama wao.
Pia,Kimanta amewataka viongozi wa mila kuacha kusimamia mila na desturi zinazochochea unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto bali wafuate taratibu na sheria zilizopo.
Akisoma taarifa ya dawati la jinsia kutoka jeshi la Polisi Nadhimu wa Jeshi Inspeta Mary Kipesha,amesema dawati la jinsia limefanya kazi kubwa katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unapungua kwa kiasi kikubwa.
Amesema kwa mwaka 2019 jumla ya matukio yaliyolipotiwa katika dawati la jinsia yalikuwa 4,305 na kwa mwaka 2020 matukio yamepungua kufikia 4,191 ambayo hii ni pungufu ya matukio 114.
ACP Mary amesema, matukio ya ukatili wa kijinsi yalipungua kwa kiasi kikubwa ni pamoja na utelekezaji wa familia kwa matukio 32, kujaribu kubaka matukio 40 na utoaji mimba matukio 39.
Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo baina ya Jeshi la polisi na taasis nyingine za serikali na binafsi.
Amesema mbali na mafanikio hayo ya kupunguza ukali wa kijinsia pia Jeshi la Polisi limeweza kuanzisha clabu mbalimbali katika shule za msingi na sekondari za kupinga ukatili wa kijinsia, pia kuanzishwa kwa kituo cha pamoja (One stop Centre) ambacho kimarahisisha utoaji huduma kwa ushirikiano zaidi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa