Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametembelea soko la Masai (Masai Market) na kuzungumza na wajasiriamali wa mapambo na bidhaa za kitamaduni na vinyago akiahidi kuendelea kutengeneza mazingira mazuri ya wajasiriamali hao kufanya biashara zao kikamilifu na kwa faida.
Mkuu wa Mkoa amesema tayari eneo limetengwa kwaajili ya wafanyabiashara hao, huku pia akiahidi kutenga eneo rasmi kwaajili ya wafanyabiashara wa soko la kwa Mrombo ili waweze kuuza vitoweo katikati ya Jiji la Arusha kama sehemu ya kukoleza utalii wa Arusha.
Mhe. Mkuu wa Mkoa katika hatua nyingine amewasisitiza wafanyabiashara hao kuendelea kuwa wakarimu kwa wageni hasa watalii ambao ndiyo Wateja wao wakuu akiwataka pia kuwa mabalozi wa Utalii kwa kuwafahamisha vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana mkoani Arusha.
Kwa Upande wake Bw. John Tarimo Mwenyekiti wa Wajasiriamali wa soko hilo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Milioni 200 kwaajili ya mikopo kwa wajasiriamali hao na kumuomba Mhe. Makonda kuwasaidia zaidi katika kuimarisha zaidi ulinzi na usalama mkoani Arusha kwani bado kuna matukio ya wizi na udokozi kwenye maeneo ya Katikati ya Jiji ambapo wageni wengi wamekuwa wakiibiwa na vijana wanaojulikana kama Tatumzuka.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa