Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewasihi wanafunzi wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) wilaya ya Arumeru kuwa na nidhamu na kuzingatia masomo kwa kuwa Serikali inawategemea kuja kulitumikia Taifa lao kwa utalamu watakaoupata chuoni hapo.
Mhe. Makonda ametoa rai hiyo, mara baada ya wanafunzi hao kuishukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Haszan kwa kuwaongezea fedha za matumizi 'boom' pamoja kuboresha miundombinu ya chuo hicho, wakati mkuu huyo wa mkoa alipotembelea chuoni hapo na kupata wasaa wa kuzungumza na wanachuo hao, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo mapema leo Mei 29, 2024, inayokwenda kwa jina la 'Siku 6 za Moto Arusha'.
Ameweka wazi kuwa, Serikali ya awamu ya sita imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira rafiki huku ikiwa na tegemeo la kupata watalamu wa fani hiyo muhimu kwa maendeleo ya Jamii ya watanzania huku akiwatia moja kuweka juhudi kwenye masomo kwa kujiamini na kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
"Nimekuja hapa kwa lengo la kusalimiana nanyi kama wakazi wa Arusha, nikiwa kama mkuu wenu wa mkoa pamoja na kuwashukuru kwa uzalendo wenu mnaojitoa kila mara kwenye matukio ya kimkoa, ninachotaka wanafunzi wote mjiamini, muwe na nidhamu itakayowapa nafasi ya kuweka mipango yenu thabiti ya maisha yenu ya baadaye, niwahakikishie mnasoma kwenye mkoa mzuri, mkoa wa watu wenye hela na mkoa wanaoishi wajanja msitamani kuondoka Arusha". Amesema Mhe. Makonda
Aidha, amesema kuwa kila mwananchuo anatakiwa kuwa na malengo ya kuja kulitumikia taafa lake huku akijipanga kufaidi matunda ya nchi yake, na kuhakikisha na kuwasisitiza umuhimu wa kupambana katika kutimiza ndoto zao kwa kuwasimulia historia ya Maisha yake na namna alivyofanikiwa kutimiza malengo aliyokuwa nayo.
Hata hivyo amewaahidi kufanya tamasha la vyuo vyote vya elimu ya kati na juu vya mkoa wa Arusha, tamasha ambalo litatoa futsa ya kila chuo kuonyesha ubunifu wa kazi wanazozifanya kwenye vyuo vyao na baadaye kufanya bonanza la shangwe kwa pamoja.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa