Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, amemuomba Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kushirikiana katika kukuza sekta ya Utalii Arusha kwa kuwa mkoa wa Arusha na Zanzibar inategemeana kiutalii.
Mhe. makonda, ametoa ombi hilo wakati akitoa salamu za Mkoa wa Arusha kwenye semina ya WanaHisa wa Benki ya CRDB Group iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha Mei 17, 2024 jijini Arusha.
Amefafanunua kuwa, kwa kuzingatia agizo alilopewa hadharani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiapishwa, agizo la kushughulikia masuala ya utalii na kuhakikisha Utalii unaimarika na kukua Arusha.
"Mhe. Rais, wewe ni ndugu yangu, ninatambua Arusha na Zanzibar zinategemeana katika sekta ya utalii na hili hatuwezi kulikwepa kutokana na ukweli kuwa watalii wanaokuja Tanzania hutembelea Arusha na Zanzibar, nikuombe kila mtalii anayekanyaga Zanziba hakikisha anafika Arusha.
Amesema kuwa, anatambua kazi kubwa inayofanyika Zanzibar katika sekta ya Utalii, ikiwa ni pamoja ujenzi wa Hoteli kubwa na kutumia fursa hiyo kumuomba Dkt. Hussen Mwinyi, kuwashawishi wawekezaji hao, kuwekeza pia mkoani Arusha, kutokana na upungufu wa vyumba vya kulala wageni kutokana na ongezeko la idadi kubwa ya watalii wanaofika mkoani Arusha, ikiwa ni matokeo ya program ya Tanzania 'The Royal Tour'.
"Licha ya kuhakikisha watalii wanaotua Zanzibar wanafika Arusha, tuwashawishi wawekezaji wa Hoteli Zanzibar kufungua matawi Arusha, jambo ambalo litachochea ukuaji wa utalii Arusha na Zanzibar kwa manufaa ya Taifa letu la Tanzania"
Hata hivyo, Mhe. Makonda ameishukuru Benki ya CRDB kuchagua Arusha kufanya mkutano mkubwa wa wanaHisa pamoja na ushirikiano mkubwa wanaotoka kwa mkoa wa Arusha.
Ikumbukwe kuwa, Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassa alipomuapia Mhe.Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa, alimuagiza kwenda Arusha kuchochea sekta ya Utalii, agizo ambalo tayari ameanza kulitekeleza kwa vitendo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa