Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewasili kwenye Ofisi za Chama Cha Mapinduzi, wilaya ya kichama ya Arumeru na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM Arumeru Ndugu Noel Severe na kuzungumza na Maafisa na viongozi wa CCM muda mfupi kabla ya kuanza ziara yake kwenye halmashauri ya Arusha, na kusisitiza kutokurudi nyuma kwenye mapambano dhidi ya wazembe na wabadhilifi mapema leo Mei 28, 2024.
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo mara baada ya kupata salamu za pongezi kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Arumeru, wakimtaka kutokurudi nyuma katika kuhakikisha Ilani ya Chama na maelekezo ya Serikali ya awamu ya sita yanatekelezwa kikamilifu na wasaidizi wake ngazi ya Mkoa.
Ameweka wazi kuwa, kamwe hatoacha kuwafichua na kuwawajibisha wazembe, wabadhirifu na watendaji wavivu wanaokwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo na kutaka aachiwe wakosoaji hao kwani anawamudu kikamilifu.
"Kelele za ukosoaji unaoelekezwa kwangu zinampa ari na nguvu zaidi ya kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi wa Arusha na kuhakikisha haki inatendeka"Amesema
Hata hivyo, Mhe. Makonda amekiomba Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuwa jicho la kubaini na kueleza kuhusu kukwama kwa miradi mbalimbali na kuwataja kwa majina watendaji vikwazo wanaozembea katika kuwatumikia wananchi na kutekeleza ilani ya Chama hicho tawala nchini Tanzania.
Aidha Mhe. Makonda amesema Mkoa wa Arusha unapaswa kuondokana na malumbano ya kisiasa na badala yake wawekeze kwenye uchumi kwa kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na fursa na mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji yaliyowekwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameingia kwenye wilaya ya nne miongoni mwa wilaya sita za Mkoa wa Arusha ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya "Siku sita za moto" na amebainisha kuwa ataendelea kushughulika vilivyo na wazembe, wavivu na watendaji wenye kuendekeza vitendo vya rushwa na kuzalisha migogoro na kero mbalimbali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa