Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameyataka Mashirika na Asas za Kiraia, kutokuwa sehemu ya kutengeneza migogoro baina ya wananchi na Serikali yao, kwa kuacha tabia ya kumhusisha na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na masuala ambayo Serikali yake haina uhusiano nayo katika majukumu yake.
Mhe.Makonda ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa maendeleo mkoani Arusha, wanaowakilisha Mashirika na Asas za Kiraia zenye kutoa huduma za kijamii mkoani humo, mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Gran Melia, Julai 8, 2024 .
Aidha amewataka wananchi kuacha tabia ya kuzusha mambo yasiyo ya msingi na kujiepusha na mambo yanayozushwa na wasioitakia mema Serikali ya awamu ya sita badala yake kuinga mkono Serikali kwa kufanya kazi na kujiletea maendeleo.
"Tujitahidi tu na sasa hivi tunaelekea kwenye uchaguzi, yatatokea mambo mengi ya uzushi na ya kupakaziana, sisi tusiwe sehemu yao kwasababu tunaijua faida tunayoipata, ukimchafua kiongozi wa Taifa unachafua taifa lako, umechafua urithi wa Taifa lako na unaharibu uchumi wa wengine." Ameongeza Mhe. Makonda.
Mhe. Makonda amewasihi wananchi na viongozi hao kuitunza sifa ya nchi na Mkoa wa Arusha, akikumbusha kuwa hata wafadhili wanaozisaidia asasi hizo wametokana na sera nzuri zilizowekwa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ameonesha dhamira yake njema katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mkutano huo umekutanisha wawakilishi 584 wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi katika mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa