Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, amewashukuru viongozi wa chama na Serikali wakiongozwa na Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wote wa mkoa wa Arusha na watanzania wote kwa ushirikiano waliouonyesha kipindi chote cha msiba wa Hayati Edwrd Lowasa, tangu ulipotangazwa siku ya mazishi.
Mhe. Mongella ametoa shukrani hizo za dhati kwa niaba ya mkoa na Kamati ya Usalama ya Mkoa huo, kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa huo mapema leo 18 February 2024, ziwafikie wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kufanikisha shughuli ya mazishi ya mzee Lowassa.
Amesema kuwa, katika kipindi chote cha msiba kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya mkoa na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, viongozi wa Mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, uliosababisha zoezi hilo nyeti la Kitaifa kufanikiwa kwa ufanisi Mkubwa.
“Viongozi na wananchi wengi walionesha ushirikiano mkubwa, kwa Kamati ya Kitaifa iliyokuwa inaratibu Msiba huu, watalam na timu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, niwaombe tuendelee na moyo huo wa upendo hasa pale linapotokea jambo lolote kwenye Taifa letu ili kudumisha umoja na mshikamano wetu.” Amesema.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki na kuwaongoza watanzania kwenye ibada maalum ya mazishi yailiyofanyia Februari 17, 2024 kijiji cha Ngarash wilaya ya Monduli.
Awali, Hayati Edward Ngoyai Lowassa alifariki tarehe 10, Februari 2024 na kutangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa ziarani mkoani Arusha.
Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa,Jina lake Lihimidiwe
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa