Na Elinipa Lupembe.
Taasisi zinazojishughulisha na Haki Jinai, zimeshauriwa kuwaelemisha wananchi kufahamu umuhimu wa kuzitambua haki zao na namna bora ya kuzipata haki hizo, ili kuondokana na migogoro isiyokuwa ya lazima inayosababisha ukosefu na uvunjifu wa amani.
Rai hiyo, imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, wakati alipopata fursa ya kuzungumza na hadhira iliyohudhuria sherehe za Kilele cha siku ya Sheria Nchini (Law Day) mwaka 2024, ziliyofanyanyika kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ameweka wazi kuwa hitaji kubwa la watanzania ni kufahamu haki zao na namna bora ya kuzipata.
Mhe. Mongella ameweka wazi kuwa, ili kupatikana kwa haki, mwananchi mwenyewe ana nafasi kubwa zaidi ya kujitafutia kwanza taarifa muhimu kuhusu haki zake, taarifa ambazo Taasisi hizo zinapaswa kuwawezesha kuzipata kupitia elimu zinazotolewa na kuwawezesha kuzisoma kwenye Tovuti za Taasisi za Umma.
Ameweka wazi kuwa, ili kuwarahisishia wananchi, kutambua namna bora ya upatikanaji wa Haki, amezishauri Taasisi zote zinazohusika na Haki Jinai kuboresha mfumo
wa kazi zao, kwa kuziunganisha kupitia mifumo ya TEHAMA, kama inavyofanyika katika Mahakama kwa sasa pamoja na kutoa elimu hiyo kupitia mitandao inayoweza kuwafikia wananchi kwa urahisi.
"Silaha bora ya kupigania Haki ni kuelewa upatikanaji wa hiyo, Haki unayopigania ipo chini ya Sheria, Kanuni au Taratibu ipi, hivyo kutokana na uelewa wa wananchi wengi, Taasisi hizo zinawajibu wa kuboresha mifumo ya kuwafikia wananchi, ili waweze kuwa na uelewa mpana zaidi namna bora ya kupata haki zao bila kuwa na migogoro" Amesema Mhe. Mongella.
Ameongeza kuwa, ikiwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwendesha Mashtaka, Jeshi la Magereza na Polisi pamoja na Taasisi zingine zinazojishughulisha na masuala ua kisheria zitaunganisha mifumo kupitia TEHAKA, licha ya kurahisisha upatikanaji wa haki, zaidi itaongeza uwezo wa wananchi kutambua namna bora na rahisi ya kupata haki zao.
Aidha, ameipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kwa huduma zilizotolewa kwa wananchi katika wiki ya Sheria, huduma ambazo ziliwanufaisha wananchi wengi wa mkoa huo, pamoja na kuwaunganisha na kuzifahamu Taasisi zinazojihusisha na Haki Jinai, jambo ambalo limeleta uhalisia wa dhima ya Siku ya Sheria nchini, inayomlenga mwananchi na wadau wa Sheria.
"Nikiri kuwa, licha ya wananchi zaidi ya laki moja kunufaika na elimu ya masuala ya kisheria na Haki Jinai, wananchi wananchi 516, waliopata msaada wa kisheria bure ni idadi kubwa ambayo, tunaamini wananchi hao wamepata amani ya mioyo na wanakwenda kuishi kwa amani na kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali, jambo ambalo linaimarisha amani na usalama wa mkoa wetu"Amethibitisha Mhe. Mongella.
Awali, Kilele cha Siku ya Sheria, kilitanguliwa na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini, yaliyofanyika kuanzia tarehe 24 - 30 Januari, 2024, kwa kutoa Elimu kwa Umma na msaada wa Kisheria bure, kwenye viwanja TBA, eneo la Kaloleni, Jijini Arusha, yaliyobeba
Kauli Mbiu ya "Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa; Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa