Na Elinipa Lupembe
Katika kukuza na kuimarisha Sekta ya Utalii nchini, Serikali ya awamu ya sita imeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha, wananchi wanafanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa msamaha wa ushuru na punguzo la kodi kwa wawekezaji.
Hayo yamewekwa wazi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania, Gilead Terry, alipozungumza na wanahabari, muda mfupi kabla ya kuanza Kongamano la Uwekezaji, linalofanyika kwenye Ukumbi wa mkutano Gran Melia Jijini Arusha, Aprili 30, 2024.
Terry amesema kuwa, kutokana na ongezeko la idadi ya watalii inayotokana na programu ya Tanzania Royal Tour iliyofanywa na Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan mwaka 2022, imeandaa Sera inayolinda mtaji wa Mwekezaji kwa kushusha kodi kutoa dola milioni 1 mpaka kufikia laki 5 na dola elfu 50 kwa wazawa huku ikitoa msamaha wa ushuru mpaka pale mtaji utakapoanza kutoa faida.
"Tunataka mtaji wa Mwekezaji utumike kukuza mtaji wake badala ya kulipa mrundikano wa kodi, na kuruhusu kuanza kulipa kodi mara baada ya kutengeneza faida, hali ambayo licha ya kutoa unafuu kwa wawekezaji inasaidia kuvutia wawekezaji wengi zaidi wazawa na wageni kuwekeza kwenye sekta ya Utalii" Amesema Terry
Aidha, ameyataja malengo ya Kongamano hilo ni pamoja na kuwajulisha wadau fursa zinazopatikana kwenye sekta ya utalii na nafuu mbalimbali zilizowekwa na Serikali kupitia sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022 na kusisitiza wawekezaji kuwa huu ni mwaka wa kutengeneza faida kupitia sekta hiyo.
Amefafanua kuwa, Kongamano hilo litatoa fursa ya kuwasilisha fursa, zinazopatikana kwenye sekta ya utalii, mawasilisho yatakayochochea majadiliano kati ya watalamu na wadau waliopo kwenye sekta ya Utalii mkoani Arusha, ili kujua fursa na changamoto zilizopo ili kuongeza kiwango cha uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Awali, Kongamano hilo linafanyika kufuatia maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali mwanzoni mwa mwezi Aprili, 2024, akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kushughulikia changamoto ya upatikana wa vyumba vya kulala wageni.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa