Kufuatia mkakati wa Serikali wa Kuwasajili Wajasiriamali maarufu kama machinga Kidigitali, imeanza kutoa mafunzo kwa Maafisa TEHAMA, Maendeleo ya Jamii na Biashara kutoka halmashauri za Mkoa wa Arusha, ili waanze kuwasajilijili wafanyabiashara hao wadogo.
Mfumo huo utakaowezesha wajasiriamali wote, kutambuliwa, kusajiliwa na kupata Vitambulisho vya Kidijitali vitakavyowawezesha kutambulika rasmi na kunufaika na fursa za kibiashara zilizopo.
Akifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Albano Musa, Katibu Tawala Msaidizi, Mipango na Uratibu, Apolinary Seiya, amewataka Maafisa hao kufuatilia kikamilifu mafunzo hayo ili kupata ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kufanya zoezi hilo la kitaifa kwa weledi mkubwa na kufikia malengo ya Serikali ya kuwatambua wajasiriamali rasmi kwenye mfumo wa kidijitali iliyoainishwa.
Amesema kuwa, mafunzo hayo ni utekelezaji wa adhima ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wajasiriamali kutambulika rasmi ili waweze kunufaika na fursa rasmi zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi za kifedha kama vile mikopo yenye riba nafuu.
"Mfumo wa Utambuzi na usajili wa kutoa vitambulisho kwa wafanyabiashara ndogondogo umekamilika baada ya kufanyiwa maboresho makubwa ili uweze kupata vitambulisho vya kidigitali, niwatake sasa mkafanye zoezi hili kwa weledi mkubwa katika maeneo yenu bila kutoa upendeleo kwa mfanyabiashara yeyote." Amesema Seiya
Mfumo wa utambuzi, Usajili na utaoji wa vitambulisho utawezesha kuwatambua, kuwasajili na kuwapa vitambulisho vilivyounganishwa na mfumo wa NIDA, vitambulisho ambavyo vitawapa fursa ya wajasiriamali ya kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka taasisi za fedha.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Juliana Mtolela amesema kuwa, vitambulisho hivyo vitakuwa tofauti na vile vya zamani kwani vitakuwa vya kidigitali na vitakuwa na taarifa zote za muhimu za mfanyabiashara zikiwa zimeunganishwa na taarifa za vitambulisho vya NIDA na kumfanya kutambulika rasmi na Serikali pamoja na Taasisi zingine za kifedha.
Hata hivyo, washiriki wa mafunzo hayo wamethibisha kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka yanayokwenda kuwezesha kutambua mahitaji ya wajasiriamali na kutafuta namna bora ya kuwahudumia.
"Tunashukuru sana Serikali kuwezesha mafunzo haya kufanyika, yatatusaidia kupata takwimu sahihi ya wajasiriamali na wamachinga kwaajili ya kuwa na njia sahihi ya kutatua changamoto zinazowakabili sambamba na wao kunufaika na fursa mbalimbali za mikopo kutoak taasisi za fedh." Amesema Afisa Bishara Wilaya ya Monduli, Edna Fransis.
Ikumbukwe kuwa, mafunzo hayo ya mfumo huo ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa 25 Januari, 2022 ya kuunda mfumo rasmi wa kuwatambua wajasiriamali wadogo Kidigitali ili watambulike katika mfumo rasmi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa