Na Daniel Gitaro
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora , Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema matumizi ya mfumo wa PIPMS, PEPMIS na HR Assessment katika Utumishi wa Umma nchini unaenda kuondoa tabia ya majungu na uonevu katika Utumishi wa Umma huku akiwataka watumishi wa umma nchini kuupokea kwa mikono miwili mfumo huo.
Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Meru Mkoani Arusha, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS na PIPMIS) na Mfumo Maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimali watu Serikalini (HR Assessment) yanayoendelea kufanyika mkoani humo.
Amesema mfumo wa OPRAS uligubikwa na udanganyifu, uonevu na upendeleo miongoni mwa watumishi, hivyo Serikali imekuja na mfumo wa kielektoniki ili kupunguza malalamiko ya watumishi wa Umma.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Kikwete amewataka Watumishi wa Umma nchini, kufurahia ujio wa mifumo hiyo mipya kwani itatoa haki kwa wote na kuwafanya viongozi na watumishi wa Umma kwa ujumla kutekeleza majukumu yao kiuhalisia, tofauti na ilivyokuwa kwenye mfumo wa OPRAS.
Amefafanua kuwa mfumo wa PEPMIS na PIPMIS ni mwarobaini wa masuala yote yaliyokuwa yakilalamikiwa na itasaidia kwa watumishi kupandishwa vyeo kwa wakati.
Amesema kuna baadhi ya watumishi kazi yao kubwa wakifika maofisini, ni kuangalia nani kafika saa ngapi pamoja na kuchukua maneno huku na kupelekwa kwa wakuu wao ili mradi tu wapendwe.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amesema mifumo hiyo mipya inakwenda kumlazimisha Mtumishi kutekeleza majukumu yake kwa fani aliyosomea na sio vinginevyo la sivyo mfumo huo utashindwa kumtambua.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru, Mwl. Zainab Makwinya amesema mifumo hiyo imekuja wakati muafaka kwani itatoa nafasi kwa watumishi kwenda kuwahudumia wananchi na sio kukaa maofisini.
Ameongeza kuwa mfumo huo utabaini watumishi wanaokwenda maofisini kusaini tu ili waonekane wapo na wale wanaokwenda ofisini kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa