Na Elinipa Lupembe
Serikali ya awamu ya sita kupitia Ofis ya Rais TAMISEMI, imetoa magari manne ya kubeba wagonjwa na kutoa huduma za afya katika Halmashauri za wilaya ya Longido, Ngorongoro, Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru pamoja na lori moja kwaajili ya Kliniki tembezi yenye thamani ya sh. milioni 646.360 kwa mkoa wa Arusha.
Akikabidhi magari hayo kwa viongozi wa taasisi hizo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John V.K Mongella, amesisitiza kliniki hiyo tembezi ianzie wilayani Ngororongoro ili wananchi wapate huduma za afya katika maeneo yao kwa kadri ratiba itakavyopangwa.
Amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya jitihada kubwa kuboresha sekta ya afya na ndio maana ametoa magari hayo, kwaajili ya kusaidia wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo yao na kuongeza kuwa magari hayo yaliyotolewa yanapaswa kutoa huduma za afya kwa wananchi na si vinginevyo.
"Serikali ya awamu ya sita ni Serikali ya vitendo magari haya ya kubeba wagonjwa yapo matatu na jiografia ya Mkoa wa Arusha kuna maeneo yana changamoto za ufikaji wake na utoaji huduma za afya ni changamoto hivyo nawashukuru wabunge wa Mkoa huu kwa kupitisha bajeti kadhaa zilizozaa matunda haya, naomba hii kliniki inayotembea itoe huduma kwa wananchi ikiwemo madaktari bingwa wawepo ili kutatua changamoto za wagonjwa katika maeneo husika"
Amesisitiza magari hayo yatunzwe chini ya Usimamizi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa atakayepanga ratiba nzima ya mzunguko wa kliniki hiyo inayotembea kwaajili ya kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo chanjo na huduma zinazohitajika kitaalamu.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Mkombachepa ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya, ikiwemo utoaji wa magari hayo manne, ambayo yataenda kuokoa maisha ya wananchi ikiwemo wagonjwa wa dharura, wajawazito wanaojifungua na watoto wachanga wenye changamoto za kiafya.
Awali Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Emmanuel Ole Shangay ameshukuru kupata gari la wagonjwa (ambulance) na kliniki hiyo inayotembea ambazo zitaenda kuondoa changamoto za wananchi wa Ngororongoro ambao wanakaa mbali na vituo vya afya wale wa maeneo ya pembezoni.
"Tulikuwa tukipatiwa huduma za afya kwa kutumia ndege katika maeneo yasoyofikika lakini sasa hivi ndege hiyo imekuwa changamoto, gari la wagonjwa na hii Kliniki inayotembea itawezesha wananchi kupata huduma za afya kadri ratiba ilivyopangwa" Amefafanua Mbunge
Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marko Ng'umbi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwakumbuka wilaya hiyo na kuwapatia gari la kubeba wagonjwa kwani wilaya hiyo ina zaidi vituo vya afya zaidi ya vitano lakini kutokana na jiografia yake na mtawanyiko wa watu maeneo ya pembezoni ni changamoto na awali wilaya hiyo ilikuwa haina gari la wagonjwa.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ngorongoro, Lucas ole Seina amesema kuwa serikali kutoa magari hayo yataenda kuokoa maisha ya wananchi wenye changamoto za afya.
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa