Msajili wa Hazina nchini Tanzania Bw. Nehemia Mchechu amesema sheria mpya inatungwa ili kusimamia Mashirika na Taasisi za umma katika kukuza ufanisi na uwajibikaji wa Taasisi hizo kama sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
Katika sheria hiyo, Mchechu amesema miongoni mwa sehemu zitakazopewa kipaumbele ni pamoja na kuwa na mfumo wa kisheria wa upatikanaji wa viongozi wa kuongoza taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa wanapatikana viongozi sahihi kupitia mifumo sahihi na ya wazi katika kuhakikisha Taasisi na mashirika hayo yanafikia malengo.
"Ili tuwe na mabadiliko makubwa kwenye taasisi hizi za umma lazima kuwe na mabadiliko ya namna gani tunaweka Uongozi kwenye Taasisi hizi ambapo Mhe. Rais alizungumza vizuri sana umuhimu wa kuwa na watu wenye taaluma sahihi na kuwa na mifumo shindani ya kuwapa watu hao. Tunaamini kuwa Taasisi yenye uongozi imara ndiyo inayosonga mbele." Amesema.
Aidha akizungumza na wanahabari Jijini Arusha kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano AICC, Mchechu ametaja mageuzi mengine yanayosimamiwa na ofisi yake kuwa ni pamoja na usimamizi wa utawala bora, huduma nzuri kwa wateja pamoja na namna ambavyo wakuu wa taasisi hizi wanavyoishi na wafanyakazi wao na namna wanavyowaendeleza.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa