Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameagiza kupandishwa kizimbani, watendaji wa Mkoa wa Arusha waliohusika na ubadhilifu wa shilingi milioni 428 fedha zilizotengwa kutekeleza mradi kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, mradi unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF.
Mhe. Makonda ametoa agizo hilo, mara baada ya kujiridhisha na taarifa ya uchunguzi uliokuwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Arusha na kuona zipo sababu za Watendaji wote waliohusika kupandishwa kizimbani ili sheria iweze kuchukia mkondo wake.
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo, amekemea tabia ya Watendaji wabadhirifu wanaoihujumu Serikali kwa kuiba fedha za Umma na kusisitiza kuwa, hatofumbia macho mtumishi ama kiongozi yoyote atakayekwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma, ikiwemo wizi wa mali za Umma.
"Ninatoa onyo kwa watumishi wote wa Umma, viongozi wa Chama na Serikali pamoja na wananchi wote wa mkoa wa Zrusha, kujihadhari na vitendo vya rushwa kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya Utumishi wa Umma na neno la Mungu, sitaweza kumkosea Mungu wala Kiongozi aliyeniteua Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajli ya watu ambao sio waaminifu, wanaoweka mbele maslahi yao badala ya maslahi ya watanzania hususani wananchi wenye kipato duni" Amebainisha Mhe.Makonda
Hata hivyo, Mhe. Makonda ameiagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa huo, kufanya uchunguzi kwenye miradi yote saba iliyotekelzwa kupitia programu ya TASAF mkoa wa Arusha yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.7, ili kujiridhisha na taratibu zilizotumika pamoja na ubora wa miradi hiyo kwa kulinganisha na thamani ya fedha zilizotumika.
Amesisitiza pia kufanyika uchunguzi maalum kuhusu matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali kwaajili ya Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Arusha na kuahidi kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kujihusisha na wizi na matumizi mabaya ya fedha za maendeleo.
Ikumbukwe kuwa, Mhe. Makonda amefanya uchunguzi wa ubadhilifu wa fedha hizo,kufuatia malalamiko ya mwananchi kupitia video iliyozagaa kwenye mitandao ya kijamii kudhulumiwa fedha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa