Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kusimamia na kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akihitimisha kikao kazi cha kujadili Sura ya Mipango na Bajeti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa fedha 2024/25.
Suala la migogoro ya ardhi limekuwa kero kubwa kwa wananchi na njia pekee ni Viongozi hao wa mikoa kuisimamia na kutatua wakishirikiana na wataalam wao.
“kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo yenu inadidimiza shughuli za maendeleo kutokana na muda na rasilimali nyingi kutumika kushughulikia migogoro hiyo, tumieni busara na wataalamu mlionao katika Ofisi zenu katika kusuluhisha migogoro iliyopo kwa kuzingatia Sheria za Nchi, Kanuni na Taratibu” alisema Mhe. Mchengerwa.
Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kuwafuatilia baadhi ya viongozi wa Mkoa na Wilaya ambao hawafuati sheria katika kuzuia utekelezaji wa tuzo za mabaraza ya ardhi na nyumba ya Kata na Wilaya katika kutolewa kwa tuzo ya ushindi, suala ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi na mahakama yenyewe ambapo amewashauri kuwatumia vyema wanasheria wao ili kuepusha malalamiko na migongano na mhimili wa mahakama.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mchengerwa amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Adolf Ndunguru kuwasiliana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ili kuhakikisha Wakuu wa Mikoa wanapewa mamlaka ya kushughulikia kero za ardhi kwenye mikoa yao kwani pia ni msingi wa Madaraka Mikoani (Decentralization by Devolution) badala ya Maafisa Ardhi kuwa chini ya Wizara ya Ardhi jambo linalosababisha viongozi hao kushindwa kutatua migogoro mingi ya ardhi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Adolf Ndunguru akitoa maelezo ya awali amewashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kwa kazi nzuri wanazozifanya katika mikoa yao lakini pia amesema lengo la kikao kazi hicho ni kujadili utekelezaji wa mipango na bajeti kwa mwaka uliopita 2022/2023 na pia kupata mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka ujao 2024/2025, lengo pia likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kwa maana ya ufahamu wa vipaumbele vya Taifa na mikoa katika mwaka 2024/2025.
Awali akiwasilisha makisio ya bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa niaba ya Waziri wa Nchi Mhe. Mchengerwa, Bw. John Cheyo Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema jumla ya Shilingi Bilioni 247 ni makisio ya Bajeti yote ambapo Bilioni 220 ni kwa ajili ya Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Itakumbukwa kuwa mapema wiki hii, Mheshiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa hotuba kwa viongozi wateule kuhusu masuala mbalimbali likiwemo rushwa, ubadhirifu wa fedha na ukusanyaji wa mapato na Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa kwenda kuitekeleza hotuba hiyo na kusema ndio msingi wa nini wakatekeleze kwa nafasi yao.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, baadhi ya Wizara za kisekta na baadhi ya Maafisa wa Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa