Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu Makwinya amefungua Mafunzo Kabilishi kwa Mitaala iliyoboreshwa ya Elimu ya Awali na Msingi yaliyohudhuriwa na Walimu Wakuu shule za Awali na Msingi katika Halmashauri ya Meru.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa uelewa walimu kusimamia na kutekeleza Mitaala iliyoboreshwa kwa ngazi ya Elimu ya Awali na Msingi yanaendeshwa kwa siku mbili, yamefanyika kwenye Shule ya Msingi Imani Kata ya Usariver.
Aidha, Makwinya amewapongeza Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kwa utendaji kazi wao na kuwataka kutumia ofisi kama chumba cha kutatua changamoto zinazowakabili katika Shule zao.
Pia, amewataka walimu kutokata tamaa kutokana na mazingira wanayokumbana nao kwani mazingira magumu ndio yanayomuonyesha mtu utendaji kazi wake. ameyazungumza hayo akitoa ushuhuda wa yeye alivyoanza kazi mpaka alipofikia hivi sasa.
"Mimi nimeanza kazi kulikuwa hakuna majengo kama haya nimeanza kazi nikiwa Mwalimu shule inajengwa kwa kusimikwa Miti ndio wanafunzi wanasoma lakini Leo hii niko hapa, hivyo niwatie moyo ya kwamba mazingira unayofanyia kazi unaonekana na wakati mwingine tunapima uwezo wako" amesema Makwinya.
Hata hivyo, amewatakia Mafunzo mema na kuelekeza Mafunzo hayo yakawe tija kwa wanafunzi wetu kwa kuzalisha wanafunzi Bora na sio Bora wanafunzi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa