WANANCHI 604 WAJITIKOKEZA KUPATA MATIBABU YA MOYO ARUSHA
Na Prisca Libaga, Arusha
Jumla ya watu 604 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).
Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya siku tano, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge alisema asilimia kubwa ya watu waliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu a damu.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu alisema kuna wagonjwa ambao waliwakuta na shida ya mfumo wa umeme wa moyo, misuli ya moyo kushindwa kufanya kazi na kwa upande wa watoto waliwakuta na matatizo ya valvu na matundu.
“Katika kambi hii watu wote 604 tuliowaona tuliwafanyia vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo na vipimo vya maabara. Wagonjwa 83 wakiwemo watoto 21 tuliwakuta na matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi na matibabu zaidi hivyo basi tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”.
“Tumetoa elimu ya kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia watu kutokupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kutokutumia bidhaa aina ya tumbaku na kutokunywa pombe kupitiliza pia tumetoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema licha ya kutoa huduma za upimaji na matibabu kwa wananchi lakini pia wamewajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo ambao kwa sasa wanaweza kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema miundombinu iliyopo Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) iko vizuri na yote iko katika kuboresha afya ya watanzania na wananchi wa Arusha.
“Kambi hii ya matibabu hapa ALMC itakuwa endelevu, siku ya jumatatu (leo) madaktari wetu bingwa bobezi watakuwepo hapa wakitoa huduma kwa wananchi, ninawaomba wananchi mje kupima afya za mioyo yenu mapema kwa kufanya hivi kwa wale watakaokutwa wagonjwa kutawapunguza madhara katika mioyo yao na kuepukana na gharama kubwa za matibabu"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa